ATHARI ZA SWAUMU: KINAFSI, KIROHO, KIAFYA NA KIJAMII. Mwenyezi Mungu Mtukufu amewafaradhishia waislamu kufunga (swaumu) katika mw...
ATHARI ZA SWAUMU: KINAFSI, KIROHO, KIAFYA NA KIJAMII.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amewafaradhishia waislamu kufunga (swaumu) katika mwezi wa Ramadhani. Mwezi ambao imeshuka ndani yake Qur-ani Tukufu.
Ameifaradhisha
swaumu ili iwe ni ngome na kinga ya wachamungu dhidi ya shari za nafsi.
Swaumu huinasua nafsi katika maumbile yake ya kupenda mno shari na
kuivika twaa na uchamungu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia kuhusiana na swaumu:
“ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA
(swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA
ALLAH” SIKU CHACHE TU (kufunga huko)……..” (2:183-184)
Aya inafumbuliza wazi kuwa lengo la kufaradhishwa funga kwa waumini ni kuwafinyanga kuwa wachamungu.
Tena
kufunga huko ni masiku machache tu, yaani mwezi mmoja tu, mwezi wa
Ramadhani. Amesema kweli Allah, mtu ana uhuru wa kula, kunywa na kufanya
mambo yake yote ya halali katika miezi kumi na moja ya mwaka mzima na
afunge mwezi mmoja tu, Naam, ni kweli ni masiku machache lakini yenye
faida katika kipindi kizima cha mwaka.
Lengo
la masiku haya machache ni kuacha athari njema katika nafsi za
wafungaji, athari itakayodumu na kuendelea katika kipindi chote cha
mwaka.
Baada
ya mwezi huu wa Ramadhani kumalizika ionekane athari ya malezi yake kwa
waumini wafungaji yawepo mabadiliko ya wazi katika tabia na mienendo
yao.
Zoezi
la kuidhibiti nafsi na yaliyo halali liendelezwe katika kuidhibiti na
yaliyo rahamu. Swaumu ilete siha njema kwa kuunguza mafuta na ziada ya
chakula kilichohifadhiwa mwilini bila ya kutumika katika kipindi cha
miezi kumi na moja.
Muislamu ambaye anajizuilia kula chakula cha halali pamoja na kutambua kwamba maisha (uhai) yake yanategemea chakula.
Pamoja
na ukweli huu bado anakubali kuacha kula, kwa nini? Muumini anafanya
hivi kwa sababu ya kutaka radhi ya Mola wake Mtukufu kwa kuitekeleza
amri yake yenye manufaa makubwa kwake mwenyewe.
Anafanya hivyo kwa kuchelea kufikwa na adhabu kali ya Mola wake kwa kuikhalifu na kuipinga amri yake. Na anafanya hivyo kwa tamaa ya kupata rehema adhimu ya Mola wake.
Ikiwa muumini huyu ameweza na
anachokihitajia ambacho hana budi nacho ili aweze kuishi. Itakuwa ni
ajabu kwa muumini huyu huyu kushindwa kujizuia na haramu ambayo
hainamchango wowote katika uhai wake na wala haihitajiki kabisa.
Mfungaji hasemi uongo, hadanganyi, hafanyi khiyana, havunji wala
kukhalifu ahadi, hafanyi riyaa, halaani na wala hasemi ila haki na
kweli.
Mfungaji hujiepusha na utesi na usengenyi, huuzuilia mkono na ulimi wake, hufanya sana wema na huwa mkweli, mwenye kutekeleza ahadi.
Mfungaji huwa muaminifu, mwenye subira katika shida na matatizo, na huidhibiti na kuitawala nafsi yake.
Hivi ndivyo swaumu inavyomfinyanga na kumuandaa mja kuwa mchamungu katika miezi kumi na moja inayofuatia baada ya Ramadhani.
SWAUMU NI MWALIMU WA ROHO NA MLEZI WA MATASHI (MATAKWA)
Swaumu ni miongoni mwa masomo makuu ya kiamalia (pratical) ambayo hulenga kumuandaa mfungaji mkweli kuwa mchamungu.
Hulenga kumuandaa kukabiliana na magumu ya maisha ya kila siku. Kwa mantiki hii
funga huyalea matashi (matakwa), mfungaji akaweza kusema na nafsi yake
wakati inapotaka kutenda la haramu au lililo nje ya uweza wake.
Swaumu ni mwalimu
anayetoa mafunzo ya kiroho, mafunzo ambayo hupandikiza moyo wa subira
katika nafsi ya mfungaji, ili yote haya yapatikane na athariyake
ionekane ni lazima mja aitakase ibada yake hiyo, yaani afunge kwa ajili
tu ya Allah.
Kwa nini subira? Subira ina athari na umuhimu gani katika maisha yao kila siku?.
Kwa hakika swaumu (funga) si tu kujuzuia na matamanio ya tumbo (kula na kunywa) na matamanio ya tupu (jimaa).
Bali ni wajibu kujizuia na hayo kuambatana sambamba na kujizuia na tabia mbaya na baki ya madhambi mengine.
Hii ndio maana ya kauli ya Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie:
“Asiyeacha maneno ya uongo/uzushi na kuyafanyia kazi, Allah hana haja na kuacha kwake kula na kunywa” Bukhaariy.
Swaumu
kwa maana hii ni mazoezi ya kimwili na kiroho ambayo humtayarisha
mwanadamu kukabiliana na matukio ya ghafla yenye kuhuzunisha na kutia
simanzi kwa kuwa matukio kama hayo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na hapana budi yatamtokea kama si leo, basi kesho, kwa namna moja au nyingine.
Ikawa hapana budi, mwanadamu huyu aandaliwe na kupatiwa mazoezi ya jinsi ya kukabiliana na kupambana na matukio hayo pindipo yanapojitokeza tena bila ya taarifa.
Yakimtokea
asipapatike bali akae chini na kutafakari njia bora ya kukabiliana nayo
na kuyatatua. Lolote linaweza kutokea maishani, mtu anaweza kufilisika
akawa masikini baada ya kuwa tajiri asiyejua kukosa.
Inawezekana kabisa mtu
akawa mgonjwa taabani kitandani baada ya kuwa mzima mwenye siha njema
inayomuwezesha kwenda huku na kule na kufanya mambo yake yote mwenyewe.
Si
muhali mtu kuwa dhahiri mnyonge baada ya kuwa alikuwa mtu mtukufu
mwenye kuheshimika na jamii yake, leo akawa hajulikani tena wala
kutajwa.
Inatokea
mtu akawa na mke mzuri waliyependana na kuishi maisha mazuri na dhuria
(watoto) yao lakini Allah akawachukua wote na kumuacha peke yake bila ya
kuwa na wa kumliwaza. Yote hayo na mengine mfano wa haya kuna imkani ya
kumtokea mtu katika maisha.
Na ni ukweli usiopingika kwamba matukio haya yana taathira kubwa kwa nafsi.
Taathira
ambayo huweza kumfikisha mtu kutoona raha na starehe ya uhai (maisha)
huu na hivyo kufikia uamuzi wa kujitoa uhai (kujiua) ili kumuepusha
mwanadamu huyu kufika mahala hapo pabaya ni lazima apate mazoezi ya
kiamalia ya mwili na roho (swaumu) kila mwaka mara moja kwa uchache. Ili
nafsi yake iweze kuzoea kukosa inavyovipenda na kustahamili.
Mtu
kusubiri (kustahimili) kuacha kile ambacho ni halali yake ni jambo zito
sana, katika nafsi ya mwanadamu kuliko kusubiri kuacha kile kilicho
haramu.
Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa ikiwa
mtu ameweza kuitawala nafsi yake na kuacha lililo halali yake, hakuna
sababu ya kushindwa kuidhibiti nafsi yake na kuacha lililo la haramu.
Kuacha
lililo la halali kunahitaji nguvu na subira nyingi kuliko kuacha
lililoharamishwa. Mtu ambaye huitazama neema aliyonayo kwa jicho la
amana aliyopewa na Mola wake na anaweza kuichukua wakati wowote.
Mtazamo huu humsahilishia kusubiri kuondoka kwa neema hiyo na kuridhia na kusalimu amri kwa lile alilolikadiria Mola wake.
Ni
dhahiri iliyo bayana kwamba kila mwanadamu anahitaji subira katika
maisha haya. Mwanafunzi anahitajia sana subira katika kazi yake ngumu ya
kulima, ndipo aweze kuvuna matunda ya jasho lake.
Hata
rais (kiongozi) wa nchi pia anahitajia subira ya kutosha katika
kufanikisha kuiongoza nchi. Kwa ujumla kila mmoja wetu hana budi kuwa na
subira katika maisha hata kuishi na watu majumbani, makazini na hata mitaani pia kunahitaji subira.
Kwa hiyo itakudhihirikia kwamba subira ni kitu azizi na muhimu sana katika kurahisisha na kuchanganyika kimaisha.
Ni
kutokana na umuhimu na ugumu wa suala zima la subira ndio ikawa ujira
wake ni mkubwa usiojulikana ila na Allah pekee, yeye ndiye ajuaye
amewaandalia nini wenye kusubiri, tusome:
”…………….NA BILA SHAKA WAFANYAO SUBIRA (wakajizuilia na maasia na wakaendelea kufanya ya twaa) WATAPEWA UJIRA WAO PASIPO HISABU” (39: 10).
Subira hii ni mojawapo ya mafunzo na malezi yanayotolewa na chuo hiki kikuu cha nne cha Uislamu (swaumu).
Chuo
hiki kinamuandaa mwanachuo (muumini) kuwa na subira katika kukabiliana
na magumu ya maisha ikiwa ni pamoja na kuzoea hali ya kupata na kukosa.
Mwanachuo huyu akihitimu mafunzo yake ya mwezi mmoja chuoni kila mwaka hutunukiwa shahada ya juu ya subira.
Subira ambayo itakuwa ni silaha kubwa katika maisha yake ya miezi kumi na moja ifuatayo baada ya mafunzo.
Website
yako (WEBSITE UISLAMU) inazidi kuamini kuwa unaelewa sasa kwa nini
unafunga, unaelewa kuwa falsafa ya amri hii ya Mola wako, kwa hivyo
utajitahidi kufunga kama alivyoamrisha Mola wako.
ALLAH NDIYE AJUWAE ZAIDI
IMENAKILIWA NA sayyidbunduki.blogspot.com
KUTOKA KATIKA VYANZO VINAVYOAMINIKA

COMMENTS