Madhara ya ulevi kwa binadamu KILA sifa njema anazistahiki Mwenyezi Mungu ambaye amempa heshima mwanadamu na kumfanya kuwa bora kul...
Madhara ya ulevi kwa binadamu
KILA sifa njema anazistahiki Mwenyezi
Mungu ambaye amempa heshima mwanadamu na kumfanya kuwa bora kuliko
viumbe vingi (1). Na rehema amani zimfikie Mtume Muhammad aliyeletwa
akiwa ni rehema kwa viumbe
Miongoni mwa visa vya kushangaza na
kutisha ni hiki: Kijana mmoja, akiwa amelewa, aliingia chumbani kwa mama
yake na kumtaka unyumba.Mama alikataa. Kijana alichukua kisu na
kumwambia mama yake kuwa: Usiponipa unyumba nitajiua. Mama ilimjia
huruma na hivyo akajisalimisha kwa mwanae na kumpa unyumba.
Baada ya hapo kijana alikwenda kulala
chumbani kwake. Ilipofika asubuhi, kijana alihisi kuna jambo amefanya,
na hivyo akamwendea mama yake na kumuuliza: Mama, nilifanya nini mimi
jana? Mama akajibu: Hukufanya kitu.
Kijana akamng'ang'nia mama yake amwambie
na mwishoe mama akamwambia. Kijana alichukua petroli na kuingia nayo
chooni. Alijimwagia na kujichoma moto.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe
salama!
Kijana huyu amefanya makosa makubwa matatu:1.Amekunywa Pombe. 2. Amezini na mama yake. 3.Amejiua.
Kisa hiki ni miongoni mwa visa vingi
vilivyo tokea na vinavyoendelea kutokea. Kwa sababu hii, ndio maana
ulevi umeitwa Mama wa Maovu, na hasa hivyo ndivyo ilivyo.
MAANA YA POMBE
Pombe [khamri] ni kila kitu kinacho
ifinika akili kwa njia ya ladha na starehe. Mara nyingine pombe huitwa
kileo na mara nyingine huitwa vinywaji vya kiroho au alcohol au madawa
ya kulevya [mikhadarati] kwa aina zake zote. Kinacho zingatiwa ni maana
na makusudio na sio matamshi au herufi. Imekuja katika Hadithi ya Mtume
Muhammad, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani, iliyosimuliwa na
Abuu- Maalik Al-Ash'ariy kwamba alimsikia Mtume akisema kuwa: "Wallahi
[nina'apa kwa Mwenyezi Mungu kuwa] kuna watu katika umma wangu
watakunywa pombe na wataiita kwa jina lisilokuwa lake"(2)
Jihadhari ewe ndugu yangu yasije yakakutatanisha mambo kwa pombe kubadilika jina pale inapoitwa wiski[whisky] au jina jingine.
Elewa kuwa hiyo ni pombe na ni kileo hata
kama jina lake limebadiliwsha"Na kila kinacholewesha ni pombe na kila
kinacholewesha ni haramu" (3)
HUKUMU YA KUNYWA POMBE
Kunywa pombe ni haramu, bali ni miongoni
mwa madhambi makubwa. Waislamu waliotangulia [Salaf]na waliofuatia
[khalaf] wamekubaliana tangu zamani juu ya uharamu huo kwa mujibu wa
hoja ²zifuatazo:
1.Amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika
kwamba:"Enyi mlioamini, hakika si vingine isipokuwa kwamba pombe na
kamari na masanamu na ramli ni uchafu katika vitendo vya shetani. Hivyo,
jiepusheni navyo ili mfanikiwe. Hakika, si vingine isipokuwa kwamba
shetani anataka atie kati yenu uadui na chuki katika pombe na kamari na
awazuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Je,mmekoma ?" (4)Aya hizi
zilitosha kabisa kuwafanya Waislamu waache pombe bali na kuimwaga
barabarani. Ewe ndugu yangu Mwislamu, hebu angalia picha hii: Imepokewa
kutoka kwa Anas,Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, akisema kuwa: Nilipokuwa
natembeza [nagawa] glasi za [pombe] kwa Abu-Talha, Abu-Ubaida
Ibn-Aljarraah, Abu-Dujaanah, Muadh bin Jabal na Sahli bin Baidh mpaka
vichwa vyao vikawa vinayumba kutokana na [ukali wa pombe ya]mchanganyiko
wa tende na kokwa zake, nilimsikia mnadi akisema: Ee! Hakika, pombe
imeharamishwa. Amesema Anas kuwa: Kutokana na wito huo, hakuingia wala
hakutoka mtu [klabuni] mpaka tukaimwaga pombe na kuvunja mitungi. Baadhi
yetu walitawadha na wengine wakaoga kwa Ummu-Sulaim, halafu tukatoka
kwenda msikitini na kumkuta
Mtume anasoma aya hizi: Enyi mlioamini, hakika si vingine isipokuwa kwamba pombe .....(mpaka) ....je , mmekoma ?" (5)
Ewe ndugu yangu Mwislamu, hivi ndivyo
unavyokuwa msimamo wa Mwislamu katika kuitikia amri za Mola
wake.Anatakiwa kuitikia haraka, bila ya kusita wala kuchelewa au
kungojea.
Ewe ndugu yangu mpenzi, tutangaze toba
kwa Mola wetu na tukariri kama Sahaba, Mwenyezi Mungu awawiye radhi,
walivyokuwa wakikariri kusema: "Tumekoma ewe Mola wetu, tumekoma ewe
Mola wetu".
2. Sheria ya Kiislamu imelipiga vita
vikali sana ovu hili na kupelekea kuwalaani aina kumi ya watu kuhusiana
nalo.Idadi kama hii haukutajwa katika maovu yoyote mengine. Imepokewa
kutoka kwa Anas, Mwenyezi Mungu amwiye radhi, akisema kuwa: "Mtume wa
Mwenyezi Mungu amewalaani watu kumi kwa sababu ya ulevi: 1.Mkamua pombe
[mtengenezaji]na 2.Anayekamuliwa [anayetengenezewa] na 3. Mnywaji pombe
na 4.Anayebeba pombe na 5.Anayepelekewa na 6.Anayenywesha pombe(mhudumu
/mfadhili) na 7.Anayeuza pombe na 8.Anayekula thamani yake na 10. Anaye
nunuliwa pombe" (6)
Ewe ndugu yangu, pengine unaweza
kujiuliza: Nini maana ya laana? Maana ya laana ni kutengwa na rehema za
Mwenyezi Mungu. Je, unaridhia ndugu yangu kutengwa na rehema za Mola
wako? Tunamuomba Mwenyezi Mungu atulinde na hilo.
3. Kwa kulikata ovu hili katika mizizi
yake, sheria ya Kiislamu imempangia adhabu mnywaji pombe. Hilo limetajwa
katika Hadithi ya Anas, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, anayesimulia kuwa
Mtume alipelekewa mtu aliyekunywa pombe na kumchapa kwa bakora mbili
viboko arobaini. Pia alifanya hivyo Khalifa Abubakar. Ulipokuja utawala
wa Khakifa Umar, aliwashauri Sahaba na Abdulrahman bin Auf alimweleza
Umar kuwa adhabu ndogo zaidi ni viboko thamanini (80), na hivyo Umar
akaamuru kuwa mnywaji pombe achapwe viboko thamanini (80).(7)
4. Sheria ya Kiislamu imeharamisha
kiwango kichache katika kileo [hata kama hakileweshi], iwapo kiwango
kikubwa katika kileo hicho kinalewesha. Sahaba Jabir anasimulia kwamba
Mtume amesema kuwa: "Kitu ambacho kingi chake kinalewesha, basi kichache
chake ni haramu"(8)
MADHARA YA ULEVI
Ulevi una athari na madhara mengi ambayo
si rahisi kuyataja yote katika kurasa hizi chache. Vitabu na vijarida
vimeandikwa na utafiti mwingi umefanywa mashariki na magharibi.
Yanayogunduliwa kila wakati yanaonesha wazi hatari ya jambo hili na
athari zake mbaya. Haya yanaonesha utukufu wa sheria ya Kiislamu pale
ilipoliharamisha ovu hili na kuikata mizizi yake.
i.Athari ya kwanza na hatari zaidi kwa
Mwislamu ni athari katika imani. Maasi yanaathiri imani ya Mwislamu na
hivyo imani yake inapungua na moyo wake unakuwa na giza. Iwapo ni hivyo,
hebu jiulize: Hali yako itakuwaje iwapo maasi hayo ni katika madhambi
makubwa? Aidha jiulize: Hali yako itakuwaje iwapo anayefanya maasi hayo
ameahidiwa kupata laana?
ii. Athari ya pili ya ulevi ni kwa
mnywaji mwenyewe. Kileo kina madhara makubwa ya kimwili kwa kila sehemu
ya mwili wa mnywaji na kina sumu inayoathiri moja kwa
moja kwenye mfumo mzima wa mwili. Aidha,
madhara ya ulevi yanafika kwenye chembe chembe za mfumo wa ngozi na
kwenye viungo vinavyohusika na utengenezaji wa nishati; viungo ambavyo
vinapoteza uwezo wake wa kufanya kazi ndani ya saa ishirini na nne (24)
tangu kunywa funda la kwanza la pombe.
Pombe inadhuru hususan moyo ambao baada
ya muda unabadilika na kuwa mkusanyiko wa manyavunyavu yaliyokufa,
yasiyojikunja na yasiyofanya kazi yake. Hali hii huishia kwenye kushuka
kwa mapigo ya moyo na hatimae kifo. Aidha pombe husababisha vidonda vya
koo vinavyonuka na ambavyo vinaweza kusababisha kifo baada ya saa
ishirini na nne (24) tangu kuanza kwa dalili zake iwapo havitotibiwa
haraka.
Ama uhusiano wa ulevi na ugonjwa wa
saratani (cancer) sema upendavyo. Ulevi una uhusiano mkubwa na saratani
ya tumbo, saratani ya umio (eusophagus), saratani ya ini (kidney) n.k.
Maafa makubwa zaidi ni kudhurika kwa tindikali ya DNA (Deoxyribonucleic
Acid); tindikali ya ajabu amabayo ndiyo siri ya uhai na ambayo inabeba
sifa za urithi kutoka vizazi na vizazi. Pamoja na hayo kuna magonjwa
mengine mengi kama kupumbaa kwa chembe chembe za ubongo, kuvuja damu kwa
umio, tumbo, utumbo mwembamba (small intestine), kunyambuka kwa ini,
upungufu wa damu, kifua kikuu, vidonda vya mapafu na magonjwa mengine
mengi. Mara nyingine mnywaji pombe huwa anapatwa na hali inayojulikana
kama Kichaa cha Ulevi ambapo mtu anapoteza kabisa uwezo wa kujidhibiti
na hivyo kulazimika kunywa zaidi na zaidi hadi kupoteza fahamu ambapo
anaweza azinduke au asizinduke.
iii. Athari ya tatu ya ulevi ni kwa jamii. Hapa tutatosheka kutaja takwimu za baadhi ya matukio yaliyo sababishwa na ulevi.
1. Mwaka 1968 theluthi moja (1/3) ya
matukio ya kujinyonga au ya kutaka kujinyonga yaliyotokea ulimwenguni
yalisababishwa na ulevi.
2. Mwaka 1980 asilimia themanini na sita
(86%) ya makosa ya jinai yakiwemo ya kuua, na asilimia hamsini (50%) ya
matukio ya uporaji na kutumia nguvu yalisababishwa na ulevi (WHO).
3. Mwaka 1976 madhara ya ulevi yalisababisha ajali za barabarani kama ifuatavyo:
* Nchini Marekani asilimia sitini na saba 67% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi.
* Nchini Ufaransa asililmia arobaini na sita 46% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi.
* Nchini Australia asilimia hamsini 50% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi.
4. Matatizo ya kifamilia na ya kikazi. Nadhani kisa kilichotajwa mwanzo wa makala hii kinatosha kuwa ni ushahidi.
5. Hasara za kiuchumi kwa mtu binafsi na kwa taifa:
* Hasara za kiuchumi nchini Marekani kwa mwaka ni dola za Kimarekani milioni elfu arobaini na tatu( $43,000,000,000).
* Hasara za kiuchumi kwa mwaka nchini Australia ni dola milioni elfu moja na mia moja ($1,100,000,000).
HITIMISHO
Je, katika ulevi kuna faida? Je, inafaa
kutumia pombe kama dawa? Mtume, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na
amani, alikwisha yajibu maswali haya pale aliposema kuwa: "Hakika,
Mwenyezi Mungu hakufanya dawa yenu katika vitu alivyoviharamisha kwenu"
(9) Aidha huyu hapa Taariq bin Suwaid, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi,
anamuuliza Mtume kuhusu pombe anayoitengeneza kwa ajili ya dawa, na
Mtume anamjibu kwa kusema:"Hiyo(pombe ) sio dawa bali ni ugonjwa" (10)
Ama aya ya Qurani isemayo kuwa
"Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema, katika pombe na kamari kuna
dhambi kubwa na manufaa kwa watu na dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko
manufaa yake" (11)
Aya hii inamaanisha kwamba katika pombe
kuna manufaa. Tunasema kwamba manufaa yaliyotajwa katika aya hii ni ya
kiyakinifu (material benefits) kabla ya pombe kuharamishwa. Ama baada ya
pombe kuharamishwa haifai kuiuza wala kuinunua achilia mbali
kuinywa.Pia pato lake ni haramu. Iwapo Mtume anasema kuwa pombe ni
ugonjwa je, sisi tuitumie kama dawa? Sayansi za kisasa zimethibitisha
kwamba hakuna faida zozote za kiafya katika pombe bali kinyume chake ni
kwamba kuna madhara kama tulivyotangulia kutaja.
Nataraji kuwa jambo hili tumeliweka wazi.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe sisi na nyinyi uwezo wa kufuata amri
zake, kuyaacha aliyotukataza na kukoma aliyotukemea. JE, MMEKOMA?
IMENAKILIWA NA bunduki.com
COMMENTS