BAADHI YA SALA ZA SUNNA NA FADHILA ZAKE Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtu...
BAADHI YA SALA ZA SUNNA NA FADHILA ZAKE
Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.
Allah subhanahu wataala ametufaradhishia sala tano kila
siku. Sala ambazo ni wajibu wa kila muislamu kuzisali. Pia Allah
subhanahu wataala akatuwekea sala za sunna. Sala za sunna ni muhimu
sana kuzisali kwani hujaza mapengo ya sala za faradhi ikiwa zina
mapungufu siku ya Qiyama. Kwa ujumla sala ni lazima mwanadamu azisali na
tuzisali kwa unyenyekevu kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah. Umuhimu
wa sala za fardhi na faida ya sala za sunna imeelezwa na Mtume Muhammad
(swalla Allahu alayhi wasallam) katika hadithi ifuatayo : Abu Hurayrah
(Radhiya Allaahu anhu) anatuelezea kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu
alayhi wasallam) amesema: ((Kitu cha kwanza kinachohesabiwa katika
amali za mja wa Allaah siku ya Qiyaamah ni Swalah zake. Zikiwa
zimetimia, hapo tena atakuwa kaneemeka na kafuzu, na zikiwa zina kasoro
atakuwa kaanguka na kala khasara. Ikiwa pana upungufu katika Swalah zake
za fardhi Allaah Azza wa Jalla Atasema: Angalia ikiwa mja Wangu ana
Swalah zozote za Sunnah ambazo zinaweza kufidia zile zilizopungua, hapo
tena amali yake iliyobaki itaangaliwa hivyo hivyo)) [At-Tirmidhiy, Abu
Daawuud, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ahmad].
Hivyo ndugu zanguni tujihimizeni kusali sala za faradhi na
pia tuzikimbilie sala za sunna kwani zitakuja kujaza mapengo katika
sala zetu. Leo katika makala yangu hii nitazungumzia baadhi tu ya sala
za sunna na faida zake kwa uchache. Miongoni mwa hizo ni :
1- Rakaa 12 za sunna
2-Raka mbili kabla ya sala ya alfajiri.
3- Sala ya dhuha.
4- Sala ya witri.
2-Raka mbili kabla ya sala ya alfajiri.
3- Sala ya dhuha.
4- Sala ya witri.
Ama upande wa sala ya tahajjud na fadhila zake hiyo tutaiwekea makala maalum na utaweza kuisoma.
1-Fadhila ya rakaa 12 za sunna
Imesimuliwa na Bibi Ummu habibah Ramla bint Abi
Sufyan(Radhia Allahu anha) amesema amemsikia Mtume wa Allah(swalla
Allahu alayhi wasallam) akisema " Hakuna mja yoyote muislamu atakaeswali
kwa aijli ya Allah rakaa 12 kila siku kwa kujipendekeza na si za Fardhi
ila Allah atamjengea nyumba peponi” Imepokelewa na Imam Muslim.
Mwenye kudumu na kusali rakaa hizi 12 kwa ajili ya Allah na
kwa ajili ya kujipendekeza kwa mola wake basi Allah subhanahu wataala
atamjengea mja huyo nyumba katika pepo yake. Ni nani asiyetaka pepo ya
Allah ? Tuko wapi Umma wa kiislamu kuzikimbilia kheri kama hizi. Wako
wapi wenye kushindana kwa ajili ya kupata nyumba katika pepo ya Allah ?
Suala litakuja je ni zipi hizo rakaa 12 ? Jibu la suala hilo
linapatikana katika hadithi ifuatayo : Bibi Aisha(Radhia Allahu anha)
anasema " Amesema Mtume wa Allah rehma na amani ziwe juu yake " Yoyote
atakaedumu na rakaa 12 usiku na mchana ataingia peponi: rakaa 4 kabla ya
adhuhuri na 2 baada yake. Rakaa 2 baada ya sala ya maghrib, Rakaa 2
baada ya sala ya ishaa na rakaa 2 kabla ya sala ya alfajiri"(Imepokelewa
na tirmidhy,nasai na ibn majah).
2-Raka mbili kabla ya sala ya alfajiri.
2-Raka mbili kabla ya sala ya alfajiri.
Rakaa mbili kabla ya sala ya alfajiri imetajwa ndani ya
rakaa 12 za kila siku ambazo mwenye kuzisali Allah humjengea mtu nyumba
katika pepo. Ila nimeamua kwa uchache kuielezea sunna hii kwani wengi wa
watu wamekuwa wakiipuza. Pia Mtume swalla Allahu alayhi wasallam
alikuwa akiwahimiza zaidi watu kusali rakaa hizi mbili. Inasimuliwa na
Bibi Aisha kuwa” Hakuna swala yoyote ya Sunna ambayo Mtume alikua
akiitilia mkazo zaidi kama rakaa mbili kabla ya sala ya
alfajiri”Imepokelewa na Bukhari na Muslim. Rakaa 2 hizi husaliwa kabla
ya sala ya alfajiri. Na imethibiti kwamba Mtume swalla Allahu alayhi
wasallam alikuwa akisoma sura ndogo ndani ya rakaa mbili hizi.
Zama hizi watu wamekuwa wakiamka bado kwa dakika chache
kusaliwa sala ya alfajiri ndio mtu nae hukimbilia kusali. Au wengine
husali alfajiri hali ya kuwa sala tayari imeshatoka. Rakaa mbili hizi
Mtume swalla Allahu alayhi wasallam anapiga mfano wa ubora wake kuliko
dunia na vilivyomo ndani yake. Dunia ina mazuri mangapi? Ina vitu vya
thamani vingapi ? Lakini vyote hivyo haviwezi kuzidi thamani ya rakaa
mbili kabla ya sala ya alfajiri. Imesimuliwa na Bibi Aisha (radhwiya
Allahu anha) amesema Mtume(swalla Allahu alayhi wasallam)" Rakaa mbili
za sunna kabla ya sala ya alfajiri ni bora kuliko dunia na vilivyomo
ndani yake" Imepokelewa na Imam Muslim na Tirmidhi.
Wito kwa wenye kusali sala ya alfajiri na kutojihimu na
rakaa mbili hizi tusiache kukimbilia kheri kama hizi. Na wito wangu kwa
wenye kulala wakati wa sala ya alfajiri unampita jua kwamba utaenda
kuulizwa kwa Allah juu ya kila sala iliyokupita na pia unakosa nafasi za
kheri kama hizi kwa kufuata matamanio ya nafsi yako pamoja na shetani.
3- Sala ya dhuha.
3- Sala ya dhuha.
Sala ya dhuha ni sala ambayo husaliwa robo saa baada ya
kuchomoza kwa jua na mwisho wake ni kabla ya kuingia kwa adhuhuri. Sala
hii ni miongoni mwa wasia wa Mtume Muhammad swalla Allahu alayhi
wasallam kwa sahaba wake Abuu Hurayra na wengine katika masahaba. Ila ni
wasia ambao na sisi unatufaa kuufuata na kuufanyia kazi. Imesimuliwa na
Abu-Hurayra -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema:"Ameniusia Kipenzi
changu(swalla Allahu alayhi wasallam) mambo matatu: Kufunga siku tatu
kila mwezi,Rakaa mbili za Dhuha na kusali witri kabla ya kulala"
Imepokelewa na Bukhari na Muslim na pia Mtume swalla Allahu alayhi
wassalam alimuusia hayo hayo swahaba wake mwengine Abuu-Dardai radhia
Allahu anhu katika hadityhi ilopokelewa na Imam Muslim na Abu-Daud.
Sala husaliwa rakaa mbili mbili hadi kufikia nane. Na
imethibiti zaidi kuwa Mtume swalla Allahu alayhi wasallam alikuwa
akisali rakaa nne. Hii ni sunna ambayo wengi wa watu wameisahau labda
kwa sababu ya maisha au kughurika na dunia na starehe zake. Je ni yapi
malipo kwa mwenye kusali dhuha? Atakaeswali Dhuha kachukuliwa dhamana na
Allah ya kusimamiwa mambo yake kwa siku ile kama anavyosema Mtume
swalla Allahu alayhi wassalam katika hadithi ilopokelewa na Uqba bin
Amir radhia Allahu anhu kua "Amesema Allah kumwambia mwanadamu:Ewe
mwanadamu nitosheleze mwanzo wa mchana kwa rakaa nne nami
nitakutosheleza mwisho wa mchana" Imepokelewa na Imam Ahmad
.
4- Sala ya witri
Imesimuliwa na Jabir radhiallahu anhu amesema:” Amesema
Mtume sallahu alayhu wasslam “Atakaekhofu kutosimama mwisho wa usiku,
basi aswali witri mwanzo wa usiku, na anaetarajia kua atasimama mwisho
wa usiku basi na aswali witri mwisho wake, kwan witri mwisho wa usiku ni
yenye kushuhudiwa na inayohudhuriwa (na malaika) na hiyo ndo bora”
Imepokelewa na Imam Muslim, Tirmidhi na wengineo.
Sala ya witri ina faaida kubwa sana na malipo makubwa. Yatosha fadhila yake kuwa sala ya witri inashuhudiwa na malaika. Pia ni katika wasia alousia Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) kama tulivyoeleza katika hadithi iliyopita. Witri ni 1,3,5,7,11. Mtu anasali rakaa 2. Halafu anamalizia 1. Au anasali rakaa 2 halafu tena 2 halafu anamalizia moja.
Kwa ujumla sala zote zina faida kwetu waislamu. Ni wajibu wote tujihimu na kuacha uvivu katika kuzisali sala hizi. Tunamuomba Allah atujaalie miongoni mwa wale watakaosali na kukubaliwa sala zao. Na wale wenye kukumbushwa kheri na kuzikimbilia kheri hizo. Aaamin.
Sala ya witri ina faaida kubwa sana na malipo makubwa. Yatosha fadhila yake kuwa sala ya witri inashuhudiwa na malaika. Pia ni katika wasia alousia Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) kama tulivyoeleza katika hadithi iliyopita. Witri ni 1,3,5,7,11. Mtu anasali rakaa 2. Halafu anamalizia 1. Au anasali rakaa 2 halafu tena 2 halafu anamalizia moja.
Kwa ujumla sala zote zina faida kwetu waislamu. Ni wajibu wote tujihimu na kuacha uvivu katika kuzisali sala hizi. Tunamuomba Allah atujaalie miongoni mwa wale watakaosali na kukubaliwa sala zao. Na wale wenye kukumbushwa kheri na kuzikimbilia kheri hizo. Aaamin.
Allah ni mjuzi zaidi.
imenakiliwa na sayyidbunduki.blogspot.com
COMMENTS