Ulipo si tarajio, hwenda baada ya kukosa
Hwenda hata mwenzi wako, ulonae maishani
Uliitamani leo, kuwa na ile furusa
Ridhika na matokeo, ulionayo kwa sasa
Penda
ulichokipata, kaza buti songa mbele
Ulitamani uganga, ama bingwa daktari
Uwe fundi wa manyanga, au kutibu sukari
Leo una unga unga, ni fundi wa vibatari
Penda
ulichokipata, kaza buti songa mbele
Ndoto zako udereva, upige boda tu boda
Ulisoma ukaiva, lakini kazi ni shida
Leo upo USA RIVER, fundi wachonga vigoda
Penda
ulichokipata, kaza buti songa mbele
Ulipenda uongozi, ubunge ama waziri
Kuviongoza vizazi, changamoto ulikiri
Leo wakata viazi, chipsi kwa kachumbari
Penda
ulichokipata, kaza buti songa mbele
Ulilitamani jeshi, mambo mengi ulikosa
Na ulinzi shirikishi, kote kote ulikosa
Ulipenda uandishi, leo waandika posa
Penda
ulichokipata, kaza buti songa mbele
Uonapo washkaji, hutamani fani zao
Hwenda ndo chako kipaji, kweli ulisoma nao
Ulipenda utangazaji, japo redio za mbao
Penda
ulichokipata, kaza buti songa mbele
Hakuwa chaguo lako, waungulika moyoni
Ni siri ya moyo wako, wamchekea usoni
Penda
ulichokipata, kaza buti songa mbele
Ndivyo yalivo maisha, haupati kila kitu
Wengi walisha chemsha, visu vyao kuwa butu
Piga kazi changamsha,- bongo utapa tu
Penda ulichokipata,
kaza buti songa mbele
By saidi R
Bunduki.

COMMENTS