SEHEMU YA KWANZA (1)
Hii ni likizo fupi ya mapumziko ya wiki mbili ambayo
niliipata kwa viongozi wangu wa kazi. Nayo ilikuwa ni baada ya sikukuu ya Iddi
kubwa kuisha (IDD ALHAJJ). Kwakuwa familia yangu walikuwa wameshatangulia
kijijini kwa ajili ya kujumuika pamoja na wazazi, ilinibidi safari ya kwenda
niwe peke yangu.
Niliondoka mjini Mbeya majira ya saa 12 asubuji nikiwa
katika basi la kampuni ya SAULI LUXURY COACH. Safari ilikuwa ya raha na salama
bila changamoto zozote mpaka niliposhuka chalinze majira ya saa 11 jioni.
Nilipata chakula kisha kutafuta gari nyingine ya kuelekea MKATA.
 |
| Hili ni basi la SAULI LUXURY COACH ambalo nililitumia katika safari toka Mbeya mpaka chalinze. |
 |
| bunduki. com akiwa ndani ya Basi |
Mnamo majira ya saa kumi nambili jioni nilianza safari
namba mbili ya kuelekea Mkata ambapo nilifanikiwa kufika salama kabisa majira
ya saa moja na dakika 55 usiku. Kwakuwa muda ulikuwa umekwenda sana nikaona ni
bora nilale pale ili Mungu akijaalia kesho yake (jumanne) nianze safari namba
tatu ya kuelekea kijijini kwetu Mkalamo.
Kulipopambazuka nipata chai mgahawani
na kuanza safari kwa kutumia usafiri wa pikipiki (boda boda). Nilifika Mkalamo
saa tano asubuhi na kuikuta familia yangu pamoja na wazazi wangu wote wakiwa na
afya njema na furaha na hamu kubwa ya kunisubiri.
Ndugu jamaa na marafiki wote
walikuwa na hamu dhidi yangu. Nilimshukuru Mungu kwa kuwakutat wote wakiwa
vyema na wakiendelea na shughuli zao za kila siku.
 |
| Hii ni picha ambayo imepigwa wakati nikiingia kijijini kwetu MKALAMO |
 |
| Hapa ni nyumbani kwetu kwa Sheikh Rashidi Samfyomi Bunduki |
Likizo hii ilikuwa na lengo la kuwatembelea ndugu jamaa
na marafiki, waliopo Mkalamo na walioko nje ya Mkalamo kwa sababu ni wengi
ambao hatujaonana kitambo. Miongoni mwa maeneo ambayo nilikusudia kufanya ziara
ni pamoja na KWEDIHWAHWALA, MAGUNGA, KOMUNGU, KWAMSISI NA KWAMSENGA.
Nilifarijika sana kuona Madrasa yetu imeendelea sana hasa
katika uimarishaji wa majengo yake pamoja na majengo ya msikiti kama ambavyo umejionea hapo juu.
Siku ya Alhamisi tarehe 22 / 08 / 2019 nilianza ziara
yangu kwa kuelekea Kwedihwahwala kwa ndugu zangu ambao tuliachana muda mrefu
sana takriban miaka minne ilopita. Watu kama Adamu Bichuka, Mudi Kazungu, Juma mbanga,
Rashidi Kingi na wengineo ni watu ambao muda mrefu hatujaonana hivyo nikaona ni bora
kufunga safari na kwenda kuwasalimia.
Lakini pia kwakuwa nami ni mpenzi wa ng’ombe
(dufu) niliona hii ni fursa adhimu ya mimi kwenda kushiriki japo siku moja na
vijana wenzangu katika suala hili la kumsifu mtume.
Ndugu zangu walinipokea vizuri sana sana lakini pia
nilimkuta rafiki yangu Adamu bichuka akiwa amepatiwa zawadi ya mtoto mwingine
mwingine mashaallaah hivyo safari yetu ilikuwa na neema
Siku ya ijumaa ya tarehe 23 tulianza safari ya kurudi
nyumbani (Mkalamo) wenyeji walituandalia zawadi mbali mbali na kututafutia na
usafiri wa kurudi mpaka kijijini kwetu. Safari yetu ilikuwa njema sana ALHAMDU
LILLAAHI tulifika Mkalamo mnamo saa 6 na nusu mchana na kuiwahi swala ya
ijumaa.
 |
| Maandalizi kabla ya kuondoka kurudi Mkalamo |
 |
| Furaha ilikuwa ni sehemu kubwa ya maisha yetu. Mda mchache kabla ya kuondoka |
Jioni ya siku ya ijumaa niliwaomba waalimu wa madrasa
yetu pale mkalamo tufanye zoezi kidogo la burudani ya dufu angalau kidogo
nikumbuke zamani. Basi nao bila khiyana walinikubalia na kufanya kama
tulivopanga na jambo lilikwenda vizuri sana.
 |
| Hawa ni baadhi ya vijana wangu wa Madrasa Maawa Mkalamo Handeni. wakiwa na mwalimu wao Maneno. |
Siku ya jumapili ni siku ambayo kulikuwa na shughuli ya
maulidi ya kuwarehemu wazee wetu walotangulia akhera. Maulidi hayo yalipangwa
kufanyika katika kijiji cha Magunga kata ya Kwamsisi Wilayani Handeni. Haya
yalikuwa ni maulidi ya familia (ukoo) wetu ambayo siku za nyuma yalikuwa
yakifanyika katika kijiji cha Komkonga. Hivyo basi ile likuwa ni fursa nyingine
kwa upande wangu kwa ajili ya kuonana na ndugu na jamaa wengine badala ya
kumtembelea mmoja mmoja kwake. Niliondoka asubuhi na mama watoto tukielekea Magunga kwa ajili ya shughuli hiyo. Kutoka Mkalamo Mpaka kijiji cha Magunga ni mwendo wa takriban kilomita kumi tu hivi.
 |
| Hapa shuguli ikiwa imeanza Rasmi. |
 |
| Shughuli ikiwa wakati wa kiyamu. |
 |
| Sheikh Hamis Samtoro akitoa mawaidha baada ya SHUGHULI kuisha. |
 |
| Sheikh Samfyomi akiutoa mawaidha baada ya Samtoro kumaliza |
Nilipanga kuanza safari ya kurudi Mbeya mnamo tarehe 28
lakini nilipewa taarifa ya uwepo wa Kikao kwa baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni
yetu. Hivyo kwa kuwa tarehe za kikazo zilikuwa zimekaribia sana na kikao
kilikuwa kifanyike Arusha, basi wakuu wa kazi wakasema ni bora nibaki mpaka
tarehe 31 tukutane Arusha na kumaliza kikao kabisa na hatimaye kurudi Mbeya.
Hilo kwangu lilikuwa jambo jema.
Kwa leo nitaishia hapa, nitakuwa kuendelea na sehemu ya
pili ambayo itahusisha safari ya kwenda Arusha na kurudi kwangu Mbeya.
Asante kwa kuwa nasi.
COMMENTS