Mtunzi anatufumba, amezungumzia HIZI hatujui amemaanisha nini. Lakini kila mtu ana tafsiri yake

Zinani hizi nanii, mbona zinapendwa mno
Zinatutoa nishai, kibogoyo / wenye meno
Nakubali sikatai, nitakupa na mifano
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Wameuwana wa kale, sababu ya hizi hizi
Uchawi kwa misukule, vizazi hadi vizazi
Wamechukuana nywele, kufungiana hirizi
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Kila siku makelele, mitaani hayaishi
Wana hawaendi shule, hizi zinawashawishi
Sio huyu wala yule,
maneno hayawaishi
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Mwanzo wa ngoma ni lele, lele mama lele mama
Bora yacheze machale, mapema uanze goma
Ukisema ngoja nile, nawe zitakusakama
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Hugombana hata ndugu, hizi hazimwachi mtu
Zinachochea vurugu, hazimwachi mtu katu
Hata majambazi sugu, uwe mtu au fyatu
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Pale ukishazijua, kuziacha hutotaka
Mateka waweza kua, kila siku kuzisaka
Hazichoshi abadia, hadi tutapo kuzika
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Zi tamu shinda asali, usisikie porojo
Hakuna yake mithili, zimeuzidi urojo
Hata ukiwa mkali, kwake watuliza fujo
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Madini aina gani?, mbona zinatutikisa?
Sijui mdalasini?, sijui ukweli hasa
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Au zimetiwa nazi?, kuungwa na tui bubu
Sijui ni tangawizi?, tamu ye shinda zabibu
Bado zinanipa kazi, nawaza sipati jibu
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Nisaidie mwandani, saidi nipate jua
Siri yake kitu gani?, mbona inanisumbua
Bado ningali swalini, jibu nalisubiria
Hizi zimetiwa nini?, mbona hizi zina visa?
Swali.
Je?
HIZI ninini?
Weka comment yako hapo chini.
Weka comment yako hapo chini.
By
Saidi R. Bunduki.
COMMENTS