Kuna muda unaweza ukawaona marafiki wote ulionao hawako sahihi. Ndipo nikaamua kuandika shairi hili
1. Bado namsaka hasa, mkweli muaminifu
Tangu zama hadi sasa, bado sijafua dafu
Rafiki wa kuniasa, sio wa kuleta bifu
Nani rafiki wa kweli?
2. Nilimuamini issa, tulikuwa moja safu
Nikampa zangu hisa, sikuona hitilafu
Leo kanitenda visa, na kunichezea rafu
Nani rafiki wa kweli?
3. Bado kamwe sikususa, wala sikupata hofu
Nikampata mkwasa, nikamwona mnyoofu
Kumbe yu anipapasa, aje nitoa mnofu
Nani rafiki wa kweli?
4. Rafiki wa kweli pesa, walinena wakisifu
Na hayo nikayanasa, kuyatanua mapafu
Leo pesa zanitesa, zimenitoa sharafu
Nani rafiki wa kweli?
5. Nikaiomba ruhusa, kwa walio maarufu
Mapenzi kusaka sasa, kwa heri na ubunifu
Niliteswa sikutesa, na pia kunikashifu
Nani rafiki wa kweli?
6. Penzi lilinitikisa, lilinipa usumbufu
Aliniumiza hasa, yule niliye msifu
Aliniacha kabisa, bila kunitaarifu
Nani rafiki wa kweli?
7. Iwazi yangu kurasa, nasaka wa kurudufu
Au nijaze siasa, ccm ama kafu?
Ndugu zangu wanyakyusa, wanasema mbombo ngafu
Nani rafiki wa kweli?
Mtunzi - saidi R. Bunduki
Penzi lilinitikisa 😂
ReplyDeleteHa ha haaaa
Delete