Usiku ni muda ambao ni mahususi kwa ajili ya kupumzika. Lakini ALLAH ameuwekea BONUS muda huu kwa ambao watautumia kwa ibada
- SWALA ZA USIKU NI ZIPI?
- NI MUDA GANI ULIOKUSUDIWA?
- FAIDA ZAKE
- UGUMU WAKE
- WITO KWA WAUMINI
SWALA ZA USIKU NI ZIPI?
Katika ibada ambazo ni za faradhi ziko ambazo huswaliwa wakati wa usiku kama vile Magharibi, Insha na Subhi. Lakini ni swala ambazo ni lazima kwa muislamu yeyote kuziswali.
Swala za usiku ambazo tumezikusudia hapa ni swala za Sunna ambazo hutakiwa kuswaliwa usiku wa manane maarufu kama TAHAJJUD (Kisimamo cha usiku)
Lakini mbali na Swalati Tahajudi pia ziko swala kama Tasbihi, witri na nyinginezo nyingi.
Kutokana na ugumu wake swala hili zimepewa umuhimu wa juu sana kwa ambaye atadumu nazo. Japo watu wengi wamekuwa wakishindwa kuziswali. (Allaah atuwafikishe tuwe miongoni mwa wenye kuziswali.
NI MUDA GANI ULIOKUSUDIWA?
Muda maalum uliokusudiwa kwa ibada za usiku ni nusu ya tatu ya usiku. Tukisema nusu ya tatu ya usiku ni kuanzia majira ya saa saba hadi saa 11 kabla ya kuchomoza kwa Alfajiri.
Na ni vizuri zaidi kwa muislamu kulala kidogo kisha kuamka muda huu tofauti na kukaa macho na kusubiri muda ufike.
FAIDA ZAKE
Hapa ndipo somo letu hasa tumekusidia liwe. Kwani kama mtu hafahamu umuhimu wa jambo hua haoni faida kulifanya.
"Nakuomba uambatane nami ili kusoma baadhi ya faida
hizi chache kati ya nyingi ambazo zimeelezwa na wanazuoni wetu."
1. Huongeza imani
Huu ni muda ambao una utulivu
sana, kwa Baraka za ibada hizi na kujitoa kwa mja, ni wazi kuwa Allaah
atamuongezea imani yake.
2. Humtofautisha Muislamu na muumini
Kufikia daraja ya kuwa
muumini zinahitajika jitihada za ziada tofauti na ibada za faradhi ambazo
Allaah amezifaradhisha. Kwa ibada hizi za usiku ni miongoni wa ibada ambazo
humfikisha muislamu wa kawaida kufikia daraja hizo.
3. Karama kwa muumini
Karama ni katika vipawa ambavyo wamependelewa baadhi ya wachache. Kwa ibada hizi Allaah atakuruzuku kitu hiki ambacho wengi katika waislamu hawana.
Karama ni uwezo wa
kutabiri jambo na likatokea, ndoto za kweli na uwezo wa kumfahamu mtu kabla
hajajielezea alivyo.
4. Kukubaliwa kwa dua
Wakati huu ni miongoni mwa
nyakati ambazo muislamu akiomba dua kwa Allah hairudi.
5. Kumpandisha mtu daraja
Kupanda daraja ni katika
mambo ambayo ni wachache hupata nafasi hiyo. Kupandishwa daraja na Allaah
hutokana na mja kujipendekeza zaidi kwa Mwenyezimungu. Na ibada za usiku ni
miongoni mwa yanayoleta upandaji wa daraja.
6. Kuleta nuru ya uso
Kama ilivyo kwa mwenye
kufanya maasi huzimwa nuru ya uso wake, hasa maasi ya zinaa. Basi kwa watu wema
hung’arishwa nyuso zao na Mwenyezimungu kwa Baraka zake. Na mtu akibarikiwa
uangavu wa uso basi huwa hajifichi mbele ya watu wema.
7. Njia ya kumshukuru Allah
Tumetakiwa kumshukuru
Mwenyezimungu kwa mema anayotufanyia. Miongoni mwa kushukuru kwa dhati kabisa
ni kujitahidi katika ibada zake.
8. Hufungua mafundo ya shetani
Mja anapokwenda kulala
sheitwani kumfunga mafundo matatu na kumbembeleza kwa maneno matamu kuwa “LALA USIKU NI MREFU”
Hivyo;-
- Unapoamka na kumsabihi Allaah – Umefungua kifundo cha kwanza
- Unapotawadha umefungua kifundo cha pili
- Unaposwali umefungua kifungo cha tatu
9. Makazi mema Peponi
Iko pepo maalum kwa ajili wanaoswali swala za tahajudi za usiku.
10. Ni sababu ya wanandoa kurehemewa
Mke na mume wanapoamka na
kuswali usiku hurehemewa na Mwenyezimungu na kupataa Baraka njema katika ndoa
yao.
Usiamke kuswali ukamuacha mwenza wako akiwa amelala bila udhuru wowote
Kila jambo huwa na uzito wake, hasa mambo ya kheri huwa na uzito sana ukizingatia kuwa sheitwani naye ana mchango katika hilo.
UGUMU WAKE
Bila shaka utakubaliana name kuwa usiku ni muda wa kupumzika ama sivyo? Sasa miongoni mwa ugumu wa swala hizi ni kuwa zinahitajika uamke muda ambao watu wengi wanakuwa wamepumzika.
Hii ndio maana ALLAAH akaifanya bora kuliko swala nyingine zote ambazo huswaliwa muda wa kawaida. Lakini pia ni muda mgumu hasa katika maeneo ambayo yana baridi kali kwani muda huu ndipo baridi huzidi.
Lakini pia sambamba na hilo pia ni muda ambao unatisha kwa kuwa usiku unakuwa umetulia sana na hakuna kelele nyingi za vitu wala watu
Na siku zote njia ya kufanikiwa huwa ni ngumu, hakuna kufanikiwa bila kujipinda. Hivyo tujitahidi kujipinda katika hili.
Kwa mwenye kutia nia ya dhati na akamuomba Allaah hawezi kuona uzito juu ya ibada zake na kila kitu kitakuwa chepesi inshaallaah.
WITO KWA WAUMINI
Naiusia nafsi yangu pamoja na kuwausia ndugu zangu katika kujitahidi juu ya hili. Duniani tunapita na makazi yetu ni akhera hivyo tujitahidi katika njia ambazo zitatufikisha.
Hakika utukufu ni kutafuta radhi za Allaah kwa kujikurubisha katika ibada zake hasa hizi ambazo si wengi wanazifanya. Kwani m bora wa watu ni Yule mwenye kumcha Mwenyezimungu na si vinginevyo.
MWENYEZIMUNGU ndiye mjuzi zaidi
Shukran kwa shule nzuri.
ReplyDelete