Vivutio vya watalii ni vingi, huwa tunakusogezea kimoja baada ya kingine. Eneo hili linaitwa Kijungu (Mkoani Mbeya)
Kijungu ni shimo kubwa lenye mfano wa bakuli au chungu ambalo maji mengi huporomoka na kuingia hapo kabla ya kutokea upande wa pili.
Kutokana na umbo lake ambalo limefanana sana na chungu, ndio sababu ya kuitwa kijungu.
Historia yake
Hapo kale nyuma kidogo ya eneo la kijung kulikuwa na mwamba ambao unazuia maji kupita, maji yale yalikuwa yakiruka na kutua sehemu ya mbele ndio pakachimbika na kutengeneza eneo hilo.
Lakini mbali na hayo hii ni sehemu yenye masharti sana katika mila za kabila la wanyakyusa.
- Pembeni ya eneo hilo kuna kidaraja chembamba ambacho wenyeji walikuwa wakikitumia kwa kuvuka kwenda upande wa pili. Na kuvuka hapo kuna masharti yake. Ukitoka upande mmoja unatanguliza mguu wa kulia na ukitoka upande mwingine unatanguliza mguu wa kushoto.
- Itikadi zinasema kuwa, lile ni eneo la mizimu. Kama unavuka na mzigo wa chakula kama vile mahindi, mihogo, ndizi au kingine chochote ni lazima kwanza utupe chakula hicho kidogo kabla ya kuvuka. Laa sivyo chakula hicho kitaanguka na hutofanikiwa kuvuka nacho (Itikadi za kimila.
- Maji yanapoingia kwenye kijungu hutokea mbele upande wa pili. Lakini wazee wanasema kuwa kabla maji yale hajatokea pale husafiri kwanza upande wa kilomita 2.5 chini ya mlima huko na kurudi kisha ndipo hutokea pale.
- Ikitokea mtu amezama pale kwenye kijungu basi ataonekana baada ya siku 7 akiwa tayari ameshakufa.
- Mwamba wa eneo lile unateleza na ni hatari kwa watalii ambao wanatembelea na kupiga picha. Usipokuwa makini unaweza kujikuta umetumbukia ndani na kupotea.
- Huruhusiwi kuogelea mahala pale kutokana na hatari iliyopo.
- Unaruhusiwa kupiga picha na video.
Yako mengi ambayo tulijifunza na kujua historia ya eneo lile la kijungu. Hayo ni baadhi tu.
Tunaomba maoni yako chini hapo utuambie kuwa ni mahala gani ungependa tukuletee historia yake?
Asante kwa kuwa nasi
COMMENTS