Vivutio vya watalii ni vingi, huwa tunakusogezea kimoja baada ya kingine. Hili ni Daraja la Mungu Mkoani MBEYA

Kila sehemu ina historia yake, lakini baadhi ya historia hustaajabisha sana.
Umeshawahi kulisikia daraja la Mungu?
Bunduki Media ilifunga safari mpaka eneo hilo la kihistoria.
![]() |
| Pichani ni Mwandishi Saidi Bunduki na nyuma ni Daraja hilo. |
Hili ni daraja la asili ambalo hupatikana katika Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Takriban kilomita 65 kutoka Mjini Mbeya kuelekea barabara iendayo Kyela, unashukia katika Kijiji kinachojulikana kwa jina la KK (Kijiji Kitulivu).
Unaacha barabara kuu na kuingia barabara ya vumbi upande wa kulia. Mwendo wa takriban dakika 20 ukiwa kwenye piki piki. Hapo utakutana na Daraja hilo la kustaajabisha.
Tulitaka kujua mawili matatu kuhusiana na daraja hilo, na hizi ni dondoo ambazo nimekuandalia.
Daraja hili ni la miaka mingi sana tangu enzi za wakoloni (Wamisionary)
Chanzo chake ni kwamba hili ni jiwe kubwa ambalo lilikatiza katika mto Kiwira. Mto ambao hutiririsha maji yake kutoka mlima Rungwe hadi Ziwa Nyasa.
Mwamba huu una tabaka mbili. Yaani mwamba laini na mwamba mgumu.
Kutokana na maji kuwa mengi na kupita juu ya jiwe lile na kudondokea upande wa pili, basi ikatokea hali ya mwamba laini ambao ulikuwa chini kuliwa hadi kutoboka na hatimaye kutengeneza mfano wa Daraja Gumu na maji kupita chini.
Kutokana na maji kuchimba sana eneo lile limekuwa na kina kirefu sana.
Kina cha maji yake kinaweza kufikia hadi mita 150.
Juu ya daraja hilo unaweza kuvuka na kutokea upande wa pili wa mto bila tatizo wala masharti yoyote.
Wenyeji wanasema kuwa hapo zamani ilikuwa kama mtu atakuwa na kitu chochote kibaya kama uchawi na kadhalika, basi asingeweza kuvuka pale. Na hatimaye angedondoka chini na kufa.
Je? Nitaruhusiwa kuoga katika mto huu?
Kwa mgeni haruhusiwi hata kidogo kuoga pale kwa kuhofia usalama wake. Kwani mazingira ni mabovu na maji huenda kwa kasi.
Lakini pia huruhusiwi kuvua samaki katika mto ule.
Ila unaruhusiwa kupiga picha popote upendapo, kuuliza chochote na hata kunawa maji miguuni au usoni.
Unaweza kuitazama full video hapa chini
Vipi kuhusu maji yake? Yanafaa kwa matumizi?
Maji yake ni safi na unaweza kuyatumia kwa matumizi mbali mbali kama vile kunywa, kufua nguo, kuoga n.k.
Sambamba na hilo, lakini pia muongozaji alituhimiza na kufika sehemu ya juu ya mto ule ambako nayo ina historia yake. Sehemu hii hujulikana kama kijungu.
Hapa kuna maajabu zaidi ya daraja hili la mungu.
Soma: Maajabu ya kijungu huko mto kiwira Tukuyu Mbeya.
Asante kwa kutufuatilia katika makala zetu.
Je? Ulitamani makala ijayo tuzungumzie nini?

COMMENTS