Huenda unanifahamu vizuri tu,ila fahamu na mambo ambayo ninayo (Japo kwa uchache)
Huenda wewe unanijua, na kuna namna ambayo unanijua kwayo. Sasa hapa leo nimepata hamasa ya kukujuza baadhi tu ya tabia ambazo kwa hakika ninazo. Huenda unazijua kwangu au huzijui.
Yako mengi, lakini hapa nimeandika mambo 25 tu
1. SINA CHOYO
Sijajua ni sifa au ni nini hasa. Ila kitu ambacho kimewashangaza wengi kwangu ni kwamba sina choyo. Yaani naweza kuwa na shilingi mia na ukaniomba nikakupa na kubaki sina kitu.
Tabia hii ya kukosa choyo kuna kipindi inaniudhi sana
2. SIPENDI KUONGEA SANA
Hii inaweza ikawa kinyume na baadhi ya watu wanaonifahamu. Lakini ukweli ni kwamba asili yangu si mtu muongeaji. Nayo ni kwasababu sio mjuzi wa mambo mengi na ni muoga wa kukosolewa mbele za watu.
3. NAPENDA KUCHEKA MPAKA KULIA
Furaha yangu kubwa ya maisha ni kufurahi na kucheka. Ni miongoni mwa watu wmabao anaweza akacheka mpaka kutokwa na machozi.
4. MUOGA
Aisee mimi ni muoga sana hasa katika mambo ya kujaribu. Nadhani jambo hili litanichelewesha katika kufikia mafanikio na maendeleo.
5. MSAHAULIFU
Tena kwa watu na vitu. Yaani naweza kuonana na mtu leo, akija kesho nikawa nimemsahau kama ikiwa sikumuona vizuri. Lakini pia mambo kadhaa yanayonitokea huwa ni mwepesi sana kuyasahamu.
Hii imenifanya niwe mpenzi sana wa kuandika matukio ili niwe mwepesi kukumbuka. Nashkuru nimefanikiwa kwa kiasi fulani.
6. NAPENDA KUJIFUNZA
Napenda kuongeza ujuzi. Kama nikigundua una kitu ambacho kinaweza kunifaa, basi bila kuzingatia umri na hadhi naweza kuomba unijuze kama hutojali.
7. SINA NIDHAMU YA PESA
Na haya ni miongoni mwa mambo ambayo yatanifanya utajiri niendelee kuusikia katika redio na mitandao ya kijamii. Yaani nikipata pesa ndipo nitapanga matumizi na sio kupanga kabla ya kuipata.
Sasa kibaya zaidi pesa nayo mara nyingi huja na mipango yake.
8. BADO NAMUOGOPA BABA HADI LEO
Asili ya baba yangu ni mkali kiasi. Nakumbuka nilipokuwa mdogo nilikuwa namuogopa sana, Kitu ambacho kilinisaidia kufuata misingi anayoitaka yeye. Lakini woga ule ninao mpaka leo (Japo si kama kiwango kile)
Lakini bado namuogopa sana yule mzee, maana suala la kukupachika makofi mbele za watu ni kitu cha kawaida sana kwake. Ingawa najua kwa sasa haiwezekani lakini bado nachukua tahadhari kabla ya hatari.
9. NAPENDA MITANDAO YA KIJAMII
Nilianza kujua mitandao ya kijamii baada ya kumaliza mafunzo ya Kompyuta mwaka 2012, hapa nilianza kutumia mtandoa wa facebook. Na hapa ndipo nilianza kufurahia uwepo wamitandao hii.
Kwa sasa unaweza kunipata katika mitandnao tofauti tofauti kama vile
twitter, inshagram, whatsapp, facebook, telegram, tiktok, youtube na linkedin
11. NILIPENDA KUWA MWANAJESHI
Huenda huifahamu hii, nilipenda na bado napenda kuwa mwanajeshi. Na nilifanya usaili lakini nikafeli.
12. NAPENDA MZIKI
Ha ha ha
Sio saana ila muziki ni miongoni mwa burudani zangu kiasi. Zipo nyimbo ambazo zimewahi kunitoa machozi kulingana na hali ambayo nilikuwa nayo kwa wakati huo.
13. KUPENDEZA SIO ISHU KWANGU
Hii ni kawaida kwa wanaume wengi hasa wenye majukumu. Suala la kuumiza kichwa kuhusiana na kuvaa sio ishu sana. basi na kwangu ni hivo hivo. Sikumbuki mara ya mwisho kwenda sokoni na kununua nguo zaidi ya kununuliwa na mke wangu.
14. NAPENDA SANA MATEMBELE
Miongoni mwa mboga za majani ambazo nazipenda sana ni mboga aina ya matembele. Nilianza kuzipenda tangu nikiwa mdogo sana. Haijalishi yameungwa nazi au chukuchuku.
15. SINA NGUVU
Japo napenda kazi za nguvu lakini sina hizo nguvu zinazosemwa.
16. NINA HURUMA
Hii inataka kufanna na ile point ya kwanza ya kuwa sio mchoyo. Lakini pia huwa nawaonea huruma sana wenye matatizo haijalishi niwe na mjua au simjui.
17. NINA AIBU
'Ndio'
Maisha yangu yote yalitawaliwa na aibu, lakini kutokana na kazi ambazo tunazifanya inabidi uwe kauzu ili mambo yaweze kwenda. Ila katika uhalisia ni kwamba nina aibu nyingi sana jambo ambalo linanifanya niwe mzito sana kumkosoa mtu ambaye amenikosea. (Hasa akiwa na heshima kwangu)
18. NIMEHIFADHI ROBO YA MSAHAFU
Nimeona hii nishee nawe ili uniombee dua niweze kuongeza ujuzi. Msahafu (Qura) ina juzu 30. Hivyo namshkuru Mungu mpaka sasa nimehifadhi kichwani si chini ya juzu 7
19. NISHAWAHI KUMKATA MTU PANGA
Wakati nakuwa nilikuwa mtu mwenye hasira nyingi zaidi ya sasa. Nakumbuka miongoni mwa matukio niliopitia ilikuwa ni kumkata dada yangu panga la mguu. Lakinia nikiwa darasa la 3 nimewahi kumchoma mtu kalamu ya mkono na ikaingia haswaa.
20. NINA HASIRA NYINGI
Najitahidi kuepukana na hali hii, lakini ki uhalisia ni mtu mwenye hasira nyingi na maamuzi ya ajabu kwa wakati huo. Rejea point namba 19
21. NAIPENDA FAMILIA YANGU
Naamini kuihudumia familia yangu ipasavyo sio tu hujenga mapenzi kwao, lakini pia ni njia inayompendeza Mungu na baraka tele.
22. NAPENDA MAPENZI
Ha ha ha haaa.... Ndio mana nimeoa mapema ili nisipate usumbufu.
23. UANDISHI WA MAKALA NI MOJA YA NDOTO ZANGU
Moja ya ndoto zangu ni kuwa muandishi, kilichonirudisha nyuma ni kutopata elimu ya kutosha. Lakini pamoja na hayo naamini siku moja ndoto zangu zitatimia (Inshaallah)
24. SITAKI KUWA TAJIRI
Sitaki kuwa kama Bahresa, Mengi au Rostam. Kwani naamini kuwa ili kupata maisha yenye faraja ni kumshika Mungu na kuwa kipato cha kawaida sana ambacho hakitakufanya umkufuru Mungu.
Lakini pia naamini matajiri wanateseka sana katika maisha kuliko mimi na wewe.
25. NISHAWAHI KUVUTA SIGARA
Sikuwa mvutaji ila nimewahi kuvuta sigara. jambo ambalo limepelekea kutokerwa kabisa na mvutaji wa sigara wala kuchukia moshi wake.
Wengi hawawezi kukaa na mvuta sigara kwa sababu ya ile harufu ya moshi, lakini kwangu ni tofauti.
26. NIMEWAHI KUWA MGANGA WA KIENYEJI
Kwa kuwa nimeishi sana na waganga wa kienyeji ambao sitowataja. Hii ilinipelekea nami kushiriki sana katika mambo hayo.
27. NAPENDA KULA
Kuna tofauti kati ya kula na kulakula. Sasa mimi huenda nikawa sipendi kula kula, ila napenda kula hasaaa. Yaani kula vizuri... makuku, mawali, mapochopocho n.k.
28. NI MWEPESI KUMUAMINI MTU
Mpaka wakati mwingine najiogopa. Yaani naweza kukuamini kwa chochote hata kama sikujui. Sasa hii ni hatari sana na ni rahisi kudhuriwa.
COMMENTS