SURA YA KWANZA UKODISHAJI WA SHAMBA Baada ya kupata wazo la kulima, tulianza kuulizia mahala ambapo tunaweza kupata shamba kwa ajili y...
SURA YA
KWANZA
UKODISHAJI
WA SHAMBA
Baada ya kupata wazo la kulima, tulianza kuulizia mahala ambapo tunaweza
kupata shamba kwa ajili ya kukodisha. Maeneo ambayo tunafanya kazi (UHINDINI –
MBEYA) kulikuwa na jirani yetu ambae alikuwa anafanya kazi ya ulinzi katika
Bank ya Equity, ambaye alijulikana kwa jina la Shega. Kwa kuwa huyu alikuwa ni
mwenyeji wa huku tuliona ni bora kufanya mawasiliano nae afanye michakato.
Baada ya muda alitupa majibu kuwa alipata shamba maeneno fulani katika
Wilaya ya Mbozi Mkoa huu wa Mbeya. Hivyo alizungumza na jamaa zake wa huko.
Jambo lilipokuwa tayari tuliamua kwenda na kuliona hilo shamba na kufanya
makubaliano. Tulipanga siku rasmi ya kwenda huko.
Siku ya jumapili tarehe 15/10/2017 ndio siku ambayo tuliamua kwenda huko
shambani. tulianza safari majira ya saa 4 za asubuhi tukiwa watu wane ambao ni
bwana Ummari (Baba la baba), Afande Shega, Ben Oiso pamoja na Mimi (Saidi
Bunduki). Kiongozi wa safari hii alikuwa ni bwana Ummar (Baba la baba). Sehemnu
ambayo tulikuwa tunakwenda ni kijiji kiitwacho Senjele. Kijiji ambacho
kinapatikana takriban kilomita 45 kutoka Mbeya mjini kuelekea TUNDUMA.
Safari hii ilikuwa ni kwajili ya kwenda kuliona shamba ambalo tumekusudia
kukodisha kwa ajili ya kilimo cha mahindi. Tulifika Senjele majira ya saa 6 mchana na kumsubiri mwenyeji
wetu ambaye ndiye aliyekuwa amefanya michakato ya kutafuta hilo shamba. Jamaa
yule anaitwa SIMON alikuwa anatokea Songwe. Huyu ndiye alikuwa na mawasiliano
na bwana Shega. Baada ya muda kidogo alikuja na kutukuta tumekaa chini ya
muembe mdogo uliopo pale njiani kijijini.
Lakini pia kuja kwake bado haikuwa mafanikio kwa sababu, huyo bwana
ambaye ndiye mwenye shamba alikuwa hayupo, hivo bado kulikuwa na haja ya
kumsubiri na kufanyanaye maelewano kuhusu shamba. Pia muda ule tuliutumia kwa
ajili ya kwenda kuliona hilo shamba ambalo lilikuwa linasemekana kuwa lilikuwa
na ukubwa wa ekari sita. Kwa bahati nzuri shamba halikuwa mbali na bara bara
kuu ya Tunduma.
Pia tulifurahi kuona shamba likiwa katika hali nzuri sana. Hii ni kwa
sababu msimu uliopita lililimwa na baada ya hapo pia lilisafishwa kwa ajili ya
kujiandaa na kilimo cha mwaka huu. Kwahiyo halikuwa na miti wala majani. Labda
tu lilikuwa na haja ya kuchimbua tena na ng’ombe kwa ajili ya kuboresha zaidi.
Na pia kwa kuwa tulikuwa tumechelewa kutafuta mashamba, haikuwa rahisi kwa muda
ule kupata shamba kwa urahisi na hata kama tungepata isingekuwa rahisi kupata
shamba lililo karibu na makazi ya watu au barabara kama vile.
Mpaka muda huu tulikuwa watu watano, kwa sababu tayari alikuwa
ameshaongezeka jamaa mmoja (Simon). Huyu jamaa anaishi katika Kijiji
kinachoitwa NANYALA. Nanyala ni kijiji kilicho nyuma kidogo ya kile kijiji cha
Senjele. Hivi ni vijiji ambavyo vina mchanganyiko wa makabila ya Wanyakyusa na
Wanyiha. Na haya miongoni mwa makabila makubwa Mkoani Mbeya.
Picha halisi ikionesha
shamba jinsi lilivokuwa siku ya kwanza ambayo tulifika SENJELE. (Picha na Omy
Krish)
Upande mwingine wa
shamba. Kwa mbali zinaonekana nyumba za kijiji cha Senjele
Tulilikagua vema na kuridhika nalo kwa wakati huo tukimsubiri bwana
NICKSON ambaye ndiye mwenye eneo lile. Lakini baada ya kufanya mawasiliano naye
iligundulika kuwa alikuwa mbali kidogo na pale hivo aliomba kama kuna uwezekano
tufanye maelewano na mke wake. Tulifanya hivyo lakini mwishowe mke wake
alishindwa kufanya makubaliano kwa sababu
alikuwa na hofu juu ya kupunguza bei. Kwa hiyo ilitulazimu kumsubiri bwana
Nick.
Mpaka muda ule tayari ilikuwa ni saa nane za
mchana na njaa zilianza kututafuna. Hivyo ilibidi tuangalie sehemu ya kupata
chakula. Kwakweli sehemu ya kupata chakula kidogo ilikuwa ni changamoto kwa
sababu Senjele ni kijijini sana hivyo hapakuwa na migahawa ya kutosha. Lakini baadaye jamaa ambaye ndiye
alikuwa mwenyeji wetu ambaye ni SIMON alitupeleka sehemu ya pili ya mji ule
ambapo tulifanikiwakupata huduma ya chakula. Tulifanikiwa kupata wali
maharage pamoja na nyama za kuchoma za mbuzi.
Sehemu ya kupata
chakula. Hapa ni Saidi Bunduki akiwa na Ben Oiso. Hii ni sehemu ya nje ya
Mgahawa. (Picha na Omy Krish)
Baada kupata
chakula, watu wakirudi shambani kuelekea na majukumu mengine – Kutoka kushoto
ni Ben Oiso, Saidi Bunduki, Mr Shega na Simoni (Mwenye flana nyeupe)
Tulipomaliza kula chakula kile cha mchana tulirudi kule shambani na
kumkuta bwana NICKSON ameshafika na alikuwa anatusubiri. Baada ya sisi kufika tulirudi
tena shambani na tulielewana na kufika lengo. Kisha akaitwa Mwenyekiti wa
Kijiji kwa ajili ya maandikishiano.
Picha iliyopigwa kutoka juu
ikimuonesha Mwenyekiti.Huu ni Mkataba baada ya kukamilika
Akiwa katika harakati za kuandika
Mkataba wa shamba
Shamba lilikuwa na ekari sita, na kila ekari moja tulikubaliana ni
shilingi elfu 80. Lakini siku ile tulilipa pesa ya ekari moja tu na kuahidi
kulipa kiasi kilichobaki siku nyingine. Baada ya pale muda ulikuwaumekwenda
sana na tukaamua kurudi nyumbani. Tulifika nyumbani MBEYA MJINI mnamo majira ya
saa moja usiku.
Safari ile ilikuwa tamu sana kwa kila aliyehudhuria pale kwani ilikuwa ni
mfano wa safari ya watalii waliotembelea MLIMA KILIMANJARO huko Moshi. Kwani
kila mtu miongoni mwenu alikuwa na furaha na bashasha sana. Wananchi wa kijiji
kile walitushangaa sana kwani tulionekana kuwa moja kwa moja ni wageni tena
wenye pesa zao.
Kumbe ha ha haaa.
KUMALIZIA MALIPO YA SHAMBA
Siku ya jumapili
tarehe 05/11/2017. Safari hii tulikwenda mimi na Bwana Ummar kwa ajili ya
kumalizia pesa iliyobaki katika malipo ya shamba. Tulikwenda mara moja na kurudi. Safari hii tulikutana na
yule bwana Simon ambaye yeye anakaa katika Kijiji cha Songwe. Kiasi kilichobaki
kilikuwa ni shilingi laki nne (400,000/=). Tulipomaliza kuandikishiana kama
kawaida tukaingia dukani na kunywa soda kisha tukasubiri gari na hatimae kurudi
nyumbani mapema. Safari hii ya pili haikuwa na mambo mengi kama ile ya kwanza.
Ilikuwa ni kwa ajili ya kukamilisha muamala wa pesa tu.
SURA YA
PILI
KUANZA
KULIMA SHAMBA
Safari hii ilikuwa ni kwa ajili ya kwenda kufanya mipango ya kulima lile
shamba.Safari hii ilikuwa ni siku ya jumapili tarehe 26/11/2017
Washiriki katika safari hii walikuwa ni MR UMMAR na MKE WAKE, BEN OISO,
RAMADHANI CHIKUMBII, PAMOJA NA MIMI (Saidi Bunduki)
Tuliondoka Mjini Mbeya mnamo majira ya saa 5:44 asubuhi na kufika Mbalizi
saa 6 mchana. Tulikaa Mbalizi takriban muda wa lisaa ili kusubiri gari iondoke.
Ilipofika saa 6:57 mchana gari iliondoka na kufika SENJELE saa 6:40 mchana.
Safari hii ilikuwa ni kwa ajili ya kwenda kukamilisha suala zima la
ulimaji. Pia kwa kuwa kulikuwa na vibarua walikwishaanza kulima hivo tulikwenda
kutazama kazi walioifanya pamoja na kuwapelekea pesa yao. Tulipofika shambani
walikuwa wamelima kama kiasi cha ekari moja kasoro hivi. Lakini siku ile
hatukumkuta mwenyeji wetu ambaye ndiye alikuwa ametutafutia vibarua wale, na
tulipofanya naye mawasiliano alikuwa kidogo ametoka na isingekuwa rahisi kufika
kwa muda ule. Hivyo alitoa idhini kuwa pesa tuliokwenda nayo tumkabidhi mke
wake kwani angeikuta tu, nasi tukafanya hivo.Ulipofika muda wa saa nane mchana
kama kawaida tulielekea kule kule kwenye maeneo yetu ya kupata chakula cha
mchana. Na mambo yalivyokuwa siku hiyo utajionea
hapo katika ukurasa ufuatao.
Tulikaa kule shamba mpaka majira ya saa 10 jioni na kumaliza mambo ambayo
yalitupeleka kule. Miongoni mwa mambo hayo ni kuweka mikakati mizuri ya kulima.
Pia kwa uzuri zaidi wakulima walikuwa wameshaanza kazi yao. Hivyo katika pesa
ambayo walikuwa wanaitaka (200,000/=) tuliwaachia advance ya shilingi laki moja
na elfu ishirini.
Tuliondoka Senjele mishale ya saa 9:41 jioni na kufika Mbeya saa 10:50
jioni.
TANBIHI& MAELEZO YA ZIADA:-
Kama utafuatilia kwa makini utagundua kuwa kutoka Mjini mpaka shambani
palikuwa na muda wa kama lisaa hivi. Na kwa upande wa nauli ilikuwa ni shilingi
elfu mbili (2,000/=) kwa kila mtu mmoja. Kwahiyo utaona ni pesa kiasi gani
ilikuwa inatumika katika usafiri. Pia tulilazimika zaidi kusafiri siku za
jumapili kwa sababu ndio siku ambayo tunakuwa na nafasi kutokana na kazi yetu.
SURA YA TATU
UNUNUZIWA MBEGU NA UPANDAJI
Mnamo tarehe 02/12/2017 siku ya alhamisi. Alikuja bwana Simon kutoka
Songwe. Hiii ni kwa ajili ya kushirikiana nasi katika suala la ununuzi wa
mbegu. Alifika mnamo majira ya saa nane mchana. Baada ya muda aliondoka na
bwana Ummar kuelekea sokoni kwa ajili ya kufanikisha suala hilo na mambo yalikwenda kama yalivokusudiwa. Mbegu
tulizokusudiwazilikuwa ni aina mbili ambazo ni PANNAR na SEEDCO. Simon
alitangulia na ile mbegu kabisa ili iwe rahisi kwa wapandaji.
Mr. Simon (kulia) akiwa katika
duka la mbegu Aina ya
mbegu ambazo zilinunuliwa
Maeneo ya sokoni (Mwanjelwa –
Mbeya)
Ili kupunguza gharama tuliona ni bora kuenda kusaidia suala la upandaji
katika moja ya siku. Na ilikuwa ni vema zaidi kuenda kupanda siku ya jumapili.
Hivo tuliwaomba wale wapigaji mashimo waifanye kazi hiyo siku ya jumamosi.
Lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao haikuwezekana kufika katika
siku hiyo. Na badala yake alifika mtu mmoja tu tena siku ya kuamkia jumatatu.
Hivyo hatukuweza kwenda wote. Ila alikwenda kusimamia suala hilo bwana Simon
kutoka Songwe.
Na baadaye bwana Ummar na Ben walikwenda kukamilisha baadhi ya malipo tu
kwa vibarua. Hii ilikuwa ni tarehe 4/12/2017 siku ya jumatatu.
UOTAJI NA UKUAJI WA MAZAO
Tunamshukuru Mungu baada ya wiki mbili hivi mahindi yalikuwa tayari yameota
na kunawiri vizuri. Ingawa kulikuwa na baadhi ya maeneo kidogo yalikuwa
hayajaota vizuri lakini kwa asilimia kubwa shamba lote lilikuwa limeota vema.Siku
ya jumapili ya tarehe 17.12.2017 tuliamua kutembelea shamba ili kuendelea na
ukaguzi wetu kama kawaida. Kwakuwa siku hii ndio tunakuwa na nafasi ya kutosha
kutokana na kazi zetu. Hivyo tulipata fursa ya kuelekea shamba Mimi na bwana
Ummar. Kweli tulikuta hali ni nzuri kwa asilimia kubwa. Na mambo yalikuwa kama hivi;-
Baba
la baba akiwa katika ukaguzi shambani. (Picha na bunduki.com)
Kwakuwa mahindi bado yalikuwa
madogo na palizi ilikuwa bado haijashamiri. Hivyo baadhi ya wataalamu
walishauri kuwa kwa muda ule tuache kwanza. Tusipige mbolea wala dawa ya kuuwa
majani. Walishauri tusubiri kwa muda kama wa wiki mbili au tatu ili majani
yaote na tupige dawa ya kuuwa majani.
Tulisuibiri kwa muda huo na siku moja katikati ya wiki tuliamua aende mmoja
kwanza kukagua maendeleo ya shamba. Kwahiyo ilibidi Bwana Ummari na Ben Oiso
waende maramoja na kukagua maendeleo ya shamba. Na hali waliyoikuta shamba
ilikuwa kama utakavoona hapo chini katika picha. Kuna baadhi ya sehemu zilikuwa
bora Zaidi, nyingine zilikuwa wastani wakati nyingine zilikuwa zimedhoofika
zaidi.
sehemu “A” ya shamba ikiwa na
mahindi yenye afya bora.
Sehemu “B” ya shamba ikiwa na
mahindi yenye afya nzuriya wastani
sehemu “C” ya shamba ikionesha
mahindi yakiwa na afya iliyodhoofika na wakati huo huo kukiwa na majani makubwa
ambayo yalistahili kupaliliwa au kupigwa dawa.
SURA YA NNE
PALIZI,
MBOLEA NA DAWA YA KUKUZIA
Mpaka hapo sasa ulikuwa ni muda muafaka wa kufanya palizi. Na michakato
ya kuwatafuta watu wa kupalilia ilianza rasmi. Lakini kwa bahati mbaya kila
ambaye alipewa kazi ile alishindwa kutekeleza kutokana na sababu zake mwenyewe
binafsi ambazo hazieleweki. Kutokana na sababu ya kukosekana kwa vibarua kwa
muda muafaka hivyo mahindi yalianza kudhoofika taratibu hususan kwa sehemu “C” hii
ambayo ilikuwa haikuota vizuri na pia tayari ilikuwa na majani makubwa.
Baadaye tuliamua kupiga dawa ya kuuwa majani tu ili angalau kuyanusuru
mahindi haya. Siku moja tulimwambia bwana simon aje mjini huku Mbeya ili
kusaidiana katika suala la utafutaji wa dawa ya kuuwa majani. Lakini pamoja na
dawa pia tuliona ni bora kutafuta na mbolea kabisa ili wakati majani yanapigwa
dawa ili yafe, huku nako mahindi yanapigwa mbolea ili yakue. Yaani tuliamua
kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja.
Bwana Simon aliamua kuacha kazi zake na kuja mjini kama kawaida na
kushirikiana nasi katika suala la kutafuta dawa na mbolea. Kwakweli kijana huyu
ni mfano wa kuigwa kwani alikuwa anajitolea sana katika hili bila kutaraji
malipo yoyote. Ni kwamba ni mtu mwenye
msaada mkubwa sana katika kuhakikisha masuala yetu yanafanikiwa. Tulimshukuru
sana kwa msaada wake.
Picha zikiwaonyesha baadhi ya
washiriki wa zoezi la kutia mbolea wakiwa katika harakati za kuchanganya mbolea
ya UREA na DAP.
(Picha ya kushoto
ni SIMON, kulia ni SIMON na BUNDUKI)-Picha na Omy Krish
BABA la BABA (Upande wa kushoto)
akiwa na BUNDUKI (kulia) wakiwa katika zoezi rasmi la utiaji wa mbolea – shimo
hadi shimo.
Siku ya kwenda kusaidia kazi ya kuweka dawa na mbolea ilikuwa na
maandalizi ya kutosha. Nyumbani tuliondoka watu watatu MIMI, UMMAR na MKE WAKE.
Kwa kuwa kipindi hiki tulikuwa na gari ya ofisi hivyo haikuwa shida sana katika
masuala ya usafiri na usafirishaji. Tukiwa na mifuko yetu miwili ya mbolea na
vidumu viwili vya dawa tulianza safari asubuhi majira ya saa mbili. Tulipofika
sehemu inayoitwa AYASI tuliwapitia bwana SIMON na kijana wake moja. Kwahiyo
tukawa watu watano kwenye gari. Tulipofika shambani tukawapata na watu wenginne
wawili, mmoja alikuja kwa ajili ya kupiga dawa na mwingine alisaidiana nasisi
kuweka mbolea.
Huyu naye alikuwa pia anaitwa SIMON.
Jamaa aliyekuwa anapiga dawa ya
kuuwa majani (Jina limehifadhiwa)-picha na Omy krish
Katika upande wa mbolea tulichanganya mbolea za aina mbili ambazo ni DAP na UREA. Hii ni
kutokana na maelekezo ya wataalam wetu. Kazi ya kuweka dawa na mbolea ilikuwa
kubwa sana, hata ilipofika majira ya saa saba mchana watu walianza kuumwa na
njaa ingawa mamayetu (MKE
WA BWANA UMMAR) aliandaa chai na kwenda nayo kule shambani lakini mpaka muda
ule njaa ziliuma na watu kuhitaji chakula cha mchana. Hivyo tulitoka na gari
mimi na bwana Ummar na mkewake kwenda kutafuta chakula cha mchana.
Tulikwenda pale bondeni ambako huwa sikuzote ndipo tunapopata chakula cha
mchana, lakini siku ile hapakuwa na huduma yoyote ya chakula. Kwahiyo
ilitulazimu kuendelea mbele (SENJELE YA PILI) kuangalia kama tutapata mgahawa
na kupata chakula. Lakini pia hapo Senjele ya pili hapakuwa na huduma yoyote ya
chakula kwani watu wengi walikuwa wapo
Makanisani.
Tuliendelea tena mpaka mahala panapoitwa“Njia panda ya Iyula” pia tukakosa chakula na kuendelea katika
kijiji cha mbele yake kiitwacho RWANDA na hapondio tukabahatika kupata chakula.
Tulipata wali na maharage. Tulikula na kuwabebea wenzetu ambao walikuwa
wamebakia kule shambani. Baada ya kumaliza kula tunakuja kugundua kuwa kumbe
pale hotelini huwa wanauzaga na kitimoto. Duhh simchezo, tulibaki kucheka na
kuondoka.
Jua lilipozama watu walikuwa wamechoka sana. Lakini pia kazi iliyofanyika
ilikuwa ni kubwa mno. Lakini pamoja na hayo pia kulikuwa na sehemu iliyobaki
ambayo ilitakiwa kumaliziwa kesho yake. Hii ni kutokana na kuisha kwa muda, pia
dawa ilikuwa imeisha.
Kwahiyo tulirudi nyumbani kwa makubaliano kuwa kesho yake wale jamaa
waende wakamalizie na pia Ummar aende akasimamie na kuwalipa malipo yaliobakia.
Jumatatu ilikuwa ni siku iliyofuata na bwana Ummar alikwenda na Ben Oiso ili kuhakikisha
kuwa lile suala linakwenda kama lilivotakiwa. Na tunashukuru mambo yakaenda
kama yalivopangwa. Ummar na Ben walishirikiana na vibarua wale kuhakikisha
suala linakwenda vizuri. Tulimshukuru Mungu kwa kazi ile kuisha salama.
Mr Ben Oiso akiwa katika
pozi. Hii ni ile siku ya pili alipokwenda na Mr Ummar (Baba la baba)- Picha na
Omy Krish
Dawa ya kuuwa majani humwagiliwa kwa kutumia mitungi ya kumwagilia dawa
kama ulivoona katika picha hapo juu. Na dawa hii inatakiwa baada ya kumwagiliwa
kusiwe na mvua ndani ya siku ile ili iweze kufanya kazi barabara. Kwani mvua
ikinyesha kabla ya dawa kuyakausha majani huweza kuiyayusha na kutokufanya kazi
kama inavyopasa. Kwa bahati mbaya siku ile ile tu mvua ilianza kunyesha tukiwa kule kule
shambani. Kwakweli ilikuwa mtihani, kwani majani hayakuweza kuungua kama
tulivokusudia.
*************************
Siku moja bwana Ummar akiwa na BEN na ADAMU wa SMILE walikuwa wanatoka
VWAWA kwa shughuli za kiofisi. Lakini wakati wa kurudi waliona ni vema kupitia
shamba kuangalia maendeleo. Lakini kwa kweli mahindi bado hayakuwa katika hali
nzuri kwahiyo bwana ADAM alishauri tununue dawa ya kuyapa nguvu mahindi na
kukuwa kwa haraka (buster). Hivyo tuliona ni bora kufuata ushauri huu.
Jumapili iliyofuata ilikuwa ni tarehe,,,,,,,,,,,,,,tulifunga safari ya kuelekea
shambani. Tukiwa MIMI, UMMAR na MKEWAKE, ADAM (smile) pamoja
na BEN Oiso. Safari hii ilikuwa maalum kwa sababu ya kwenda kupiga mbolea ya
kubust mahindi.Tulipofika shamba hatukuwakuta wenyeji wetu hivyo tulisumbuka
kidogo kaitika suala la kupata dumu la kumwagilia pamoja na ndoo za maji.
Lakini bwana Nick (mwenyeji
wetu/mwenye shamba) alisema kuwa dumu lake lilikuwa na hitilafu ya spring ya
kumwagilia. Hivyo tutatufe spring hiyo ili tukifika tukachukue dumu hilo.
Lakini kutokana na kutofahamu kitu hicho, tulichukua kifaa ambacho
hakikuwa sahihi na ikatulazimu baada ya kufika tukaazime dumu lingine.
Baada ya kufanikiwa kupata dumu tulikwenda nyumbani kwa bwana NICK na
kuchukua ndoo na madumu na kushuka barabarani kuchukua maji. Tulipandisha maji
shambani na hatimae watu kuanza kazi kama kawaida. Bunduki ndiye alianza kubeba
mtungi kama utakavomuona hapo chini.
BABA la BABA akiwa katika shughuli
ya umwagiliaji wa dawa ya kukuzia. (Picha na
Bunduki.com)
Shughuli iliendelea kwa muda mrefu sana mpaka ilipofika majira ya saa
saba mchana watu waliamua kula chakula. Kama kawayda mama yetu tuliyekwenda
naye (MKE WA UMMAR) alitugawia chakula na kula. Baada ya kula watu waliendelea
na kazi mpaka ilipofika majira ya saa kumi na moja jioni kila mtu alikuwa hoi
bin taabani. Baada ya kumaliza kazi tuliweka alama mahala tulipoishia na
kutafuta sehemu ili kupumzika na kujiandaa na kurudi nyumbani.
Baada ya hapo tulirudi nyumbani na kufika salama
kuendelea na majukum mengine ya kujenga taifa. Pia tulitoa shukrani za dhati
kwa bwana Adam kutoka kampuni ya SMILE COMMUNICATION kwa ushirikiano wake nasi
katika kufanikisha zoezi hili. Huyu ni jirani yetu katika maeneo ya kazi hapa
mbeya, na ni mtu tunayeshirikiana katika mambo mbali mbali.
SURA YA
TANO
MATOKEO
Baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kwenda shambani, kutokana sababu mbali
mbali ikiwemo kutokuwa na nafasi, ufinyu wa bajeti, safari za hapa na pale nk.
Lakini kwakweli tulikuwa na hamu ya kwenda kukagua maendeleo ya shamba. Hatimae
siku moja mabwana wawili waliamua kwenda kuangalia maendeleo. Mr Ummar na bwana
Ben Oiso walikwenda kuangalia maendeleo. Hii ilikuwa ni tarehe 31.03.2018
siku ya jumamosi. Waliondoka mjini mnamo
saa nne ya asubuhi.
Kwakweli mahindi yalikuwa yamefikia hatua ya kuliwa barabara. Na yalikuwa
yameshaanza kunyauka kwa mbaaali. Ila kulikuwa na baadhi ya sehemu hazikua
zinaridhisha hata kidogo. Lakini pia kuna sehemu zilikuwa zinaridhisha na kutia
matumaini. Kama ambavyo uliona katika palizi kulikuwa na sehemu zilizo nzuri,
wastani na sehemu nyingine zilikuwa ni mbaya zaidi. Na pia kama unakumbuka
tulipanda mbegu za aina mbili ambazo ni SEEDCO na PANNAR. Mbegu ambayo
haikufanya
vizuri ilikuwa ni PANNAR. Sehemu ya mbegu hii ilidhoofika kutokana na
uhaba wa matunzo na si kwamba haifai.
Na mabwana hao waliporudi walileta takwimu kamili za picha kulingana na
hali waliyoikuta huko shambani. Kama kawaida tutakuonesha picha halisi za siku
hiyo walipo tembelea.
mahindi yakiwa yamedhoofika
kutokana na kuzidiwa na majani
“Baba la baba” akiwa sehemu ya
shamba ambayo mahindi yake yapo vizuri mno. Mkononi mwake amebeba mahindi
aliyoyavuna kidogo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. (Picha na Ben Oiso)
Vijana hawa
waliporudi walikuja na mahindi ya kuchoma na tukanufaika nayo kama kawaida.
Tarehe
29.04.2018 siku ya jumapili tuliamua tena kwenda shambani kuangalia maendeleo.
Na vile vile kujua kama mahindi yapo tayari kwa kuvunwa au bado.
Safari hii
tulikwenda watu wawili ambao ni mimi (Bunduki) na bwana Ummar (Baba la baba). Na
kama ulikuwa hufahamu, sisi ndio tulikuwa wenye shamba. Hivyo baadhi ya siku
tulishindwa kuwapata ndugu zetu wahisani ambao walikuwa wanatusapoti katika
safari zetu za shamba. Hii ni kutokana na majukumu yao binafsi.
Tuliondoka
stendi kuu majira ya saa 4:52 asubuhi na kufika shambani mnamo majira ya saa
6:02 mchana. Baada ya kufika tulikwenda kwa mwenyeji wetu bwana Nick lakini
hatukumkuta wala hatukukuta mtu yeyote pale nyumbani na kuamua kupandisha
shambani.
Sasa hebu jionee
mwenyewe shamba lilivokuwa likionekana kwa wakati huo.
Ukitazama kwa haraka unaweza
ukadhani ni msitu wa AMAZON huko nchini Brazil, lakini HAPANA hili ni
shamba, na huyu ni Baba la baba akikagua mahindi yaliosalia katika sehemu hiyo (Picha na
Bunduki.com)
Picha
unayoiona hapo juu ni sehemu ya shamba ambayo ilikuwa na majani mengi sana na
ni miongoni mwa sehemu ambazo zilikosa palizi kwa muda muafaka. Kwahiyo hali ni
kama hivo inavoonekana kwa kweli.
Mawazo ni sehemu ya maisha. Bunduki
akiwa katikati ya shamba wakati wa ukaguzi. Anaonekana kuwaza jambo fulani
tusilolifahamu. (Picha na Omy Krish)
Siku ile
iliisha hivo. Kisha baada ya hapo tulijiandaa na kurudi nyumbani kwa ajili ya
kujiandaa na siku ya kuvuna.
Mtihani ni
kwamba katika mbegu zile mbili, SEEDCO ilikuwa tayari imeshakauka vilivyo
wakati PANNAR ilikuwa bado kuna mahindi mabichi mabichi. Lakini kwa ushauri wa
watu wa karibu, walisema kuwa ni bora tusubiri mahindi yakauke kabisa na tuvune
kwa pamoja. Kwani kuvuna nusu nusu kungesababisha madhara kadhaa ikiwemo wizi
wa mahindi yaliyobakia n.k.
SURA YA
SITA
MAVUNO
Mwishoni mwa
mwezi wa tano na mwanzoni mwa mwezi wa sita tayari mahindi yetu yalikuwa
yamesha kauka. Na tayari ulikuwa ni muda muafaka wa kuvuna, pia baadhi ya
majirani zetu wa shambani walikuwa wameshaanza kuvuna. Lakini kwa upande wetu
ilikuwa ni vigumu kuendelea na zoezi la kuvuna kwa sababu kipindi hiki kilikuwa
ni kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hivyo tuliona ni bora tuvute subira
mpaka pale mwezi utakapokwisha.
Baada ya
kwisha kwa mwezi wa Ramadhani tulijipanga haraka kwa ajili ya kuanza kuvuna. Siku
ya tarehe 20 / 06 / 2018 sawa na siku ya jumatano zoezi lilianza rasmi.
Tulizungumza na watu ambao wangetusaidia kuvuna na siku ilipofika walianza kazi
rasmi.
Mr Ummar na
kijana wake Ramadhani Chikumbii walielekea shambani mapema asubuhi ili
kushirikiana na vijana ambao walipewa kazi ile ya kuvuna wakiongozwa na yule
kijana anayeitwa Simon kutoka kule kule
Senjele.
TANBIHI
Kama
unakumbuka katika mtiririko huu kuna Simon wawili. Wa kwanza ni Yule tulieanza
naye kushirikiana tangu tunatafuta shamba. Huyu anaishi kijiji cha nyuma kidogo
(NANYALA) kabla hujafika shambani. Na Simon mwingine ni kijana wa
kule kule kijijini.
Picha ya kunyapia ikiwaonesha
vijana wakiwa katika harakati za uvunaji – kutoka kushoto ni Simon (wa NANYALA)
na Mr Baba la baba (Picha na Ramadhan Chikumbii)
Watu wakiwa katika shughuli za
upukuchuaji wa mahindi baada ya kuvuna.
Ilikuwa ni vigumu
kumaliza shamba lote ndani ya siku moja kutokana na ukubwa pia kutokana na hali
ya majani yaliyoko shambani. Hivyo zoezi la uvunaji lilichukua muda wa siku
mbili (yaani jumatano na alhamisi). Siku ya mwisho iliwalazimu vijana hao
kutafuta mashine ya kupukuchulia mahindi kabisa ili yalale yakiwa katika
magunia. Kiukweli kazi hii ilikuwa kubwa sana hasa kwa siku hii ya pili. Lakini
walikaza moyo na kufanikiwa kumaliza kazi kama ilivyokusudiwa ingawa walirudi
nyumbani usiku.
Baada ya
kuvuna mahindi yalisombwa na kuwekwa pale nje kwa bwana Nick, hii ni kwa ajili
ya kusubiri ubebaji na kuyarudisha nyumbani.
Ilituwia
vigumu kuyaleta mahindi kwa haraka nyumbani kwasababu mbali mbali hasa uhaba wa
vyombo vya usafiri na nafasi kwa ujumla. Hii ilipelekea mahindi kukaa kwa muda
mrefu shambani. Lakini tulizungumza na kiongozi wetu wa Galaxy bwana SALIM AL
AMARY juu ya kutusaidia katika suala la usafirishaji. Lakini akasema kuwa
tuvute subia kwani pindi itakapokuja gari ambayo inaleta mzigo tutaitumia hiyo
na kuepusha/kupunguza gharama kubwa za usafirishaji.
Siku ya
jumatatu tarehe 13/08/2018 ilikuwa ni siku ambayo tuliletewa mzigo mkubwa toka
katika branch yetu ya Tanga. Mzigo huu ulikuwa na gari ya ofisi na dereva wetu
bwana Mahamud Iyaka. Kwahiyo mnamo siku ya jumanne ya tarehe 14 tulielekea
shamba na gari kwa ajili ya kuchukua mzigo wetu. Tuliondoka majira ya saa 12
jioni na kufika shamba majira ya saa moja usiku. Lakini pamoja na hayo
ilitulazimu kwenda na mifuko mingine ya kuwekea mahindi kwa sababu pale yalikuwa
yamekaa muda mrefu na mifuko ilikuwa tayari imeshachanika. Hivyo basi usiku ule
ule ilitulazimu kuyafaulisha mahindi yale na kuyatia tena kwenye mifuko mingine
na kushona. Hii ni kazi iliyotuchukua kama masaa mawili hivi. Hata ilipofika
saa tatu ya usiku tulianza safari ya kurudi watu wakiwa wamechoka sana kuwa
shunguli mbali mbali ikiwemo upakiaji.
Katika
safari hii tulikuwa watu watatu ambao ni mimi, Ummar na dereva Iyaka. Baada ya
hapo tulirudi nyumbani na kufika majira ya saa nne usiku.
Mpaka hapa
zoezi zima la shamba lilikuwa limekwisha kwa. Na muda wa kukodisha mashamba
ulikuwa umeshakaribia.
Hivyo basi:
katika riwaya hii ya “TWENDE SENJELE” ambayo ilikuwa inazungumzia kilimo cha
mahindi kwa msimu huu wa mwaka 2017/2018, itaishia hapa. Kuisha kwa kitabu hiki
ndio maandalizi ya kitabu kingine ambacho kitaandaliwa katika msimu ujao wa
mwaka 2018/2019.
Tunamshukuru
Mwenyezimungu kwa kutuwezesha kufanikisha suala hili mpaka kufikia hapa tangu
tumeanza siku ya kwanza mpaka leo.
HITIMISHO
Shukrani za dhati ziwafikie:-
-
OMY
KRISH :- Kiongozi
wa msafara / Mpiga picha / Director
-
BEN
OISO :- Mhariri
/ Afisa kilimo
-
SAIDI
R. BUNDUKI
:- Mwandishi / Mchapishaji
-
NICKSON :- Mwenyeji wetu / Aliyetukodisha shamba
-
SIMON
(Wa Nanyala)
:-Mtu aliyekuwa karibu nasi zaidi
katika
shughuli zote za shambani
-
ADAM
NGOTTA (SMILE) :-Jirani
aliyekuwa karibu nasi
-
SIMON
(Wa Senjele)
:- Aliyekuwa kiongozi wa vijana wa
kazi
kijijini (Senjele)
Bila kuwasahahu wana kijiji wote wa Kijiji cha Senjele wakiwemo
wanakwaya ambao pia walichangia katika kuzorotesha zoezi zima la palizi.
Bila kumsahau Mtendaji wa kijiji kwa kutupa ushirikiano mzuri
katika makabidhiano ya shamba na kadhalika.
Pia shukrani za dhati tunazitoa kwa Kampuni ya GALAXY COMPUTERS CO, LTD kwa
kutoa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha zoezi hili mpaka kufikia hapa ikiwemo
msaada mkubwa wa vifaa vya uandaaji wa riwaya hii, usafiri, na ushauri pia
katika kilimo.
Na mwisho shukrani ziwaendee wale wote ambao kwa namna moja au
nyingie walishiriki katika kufanikisha suala hili ambao hapa sikuweza kuwataja
bila kukusahau wewe msomaji wa Riwaya hii.
Asante.
COMMENTS